Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurekebisha baadhi ya makosa yaliyojitokeza katika utawala wa awamu ya tano.
Pamoja na hilo, amemtaka mkuu huyo wa nchi aendelee kuliunganisha Taifa na kuwasikiliza wananchi wote hukuakitambua kuwa Watanzania wanahitaji Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuwa Chadema haitapiga magoti katika kuidai hadi ipatikane.
Kwa upande wake, Rais Samia amewahi kueleza kuwa suala la Katiba mpya kwa sasa lisubiri kwanza ili kupata fursa ya kukuza uchumi.
Hata hivyo, kikosi kazi kilichoundwa baada ya mkutano wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi na vyama vya siasa kimetoa mapendekezo kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa nchini ikiwemo Katiba mpya.
Katika moja ya mapendekezo yake, kikosi hicho kimeshauri mchakato wa Katiba mpya kuanza baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2025. Mbowe aliyasema hayo jana, alipozungumza na wafanyabiashara wa mitaa ya Aggrey na Raha Square, Kariakoo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya chama hicho ya ‘Join the Chain’, yenye lengo la kuhamasisha utoaji wa michango kwa ajili ya ujenzi wa chama hicho.
“Lakini kwa sababu mama (Rais Samia) ameonyesha uungwana, lazima tumheshimu, tumezungumza naye akasema ebu tukaeni, tukamwambia sawa mama tutazungumza na tunakutana wapi au tunatofautiana wapi, inawezekana hakuna tutakapotofautiana bali ni hofu tu ya CCM kung’olewa madarakani,” alisema.
Alisema (Chadema) watalizungumza suala hilo, wakiamini watafikia mwafaka wa namna ya kwenda katika Katiba mpya bila kuingia katika misuguano isiyokuwa ya lazima.
Mwanasiasa hiyo aliwataka Watanzania kujiandaa na taratibu za majadiliano, akisema chama chake kitazungumza na Serikali, vyama vingine vya upinzani na CCM ili kutafuta njia bora ya kulipatia Taifa Katiba mpya.
Kuhusu Rais Samia, Mbowe alisema wanamheshimu kiongozi huyo wa nchi ambaye amekuwa muungwana na amekutana naye na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali.
Alisema katika utawala uliopita vyama vya upinzani vilikuwa katika wakati mgumu katika utekelezaji wa shughuli za kisiasa.
“Hata hapa Raha Square walikuwa wanakuja wana CCM, lakini leo nimekuja mpinzani. Haya mambo ndani ya miaka mitano hayajaonekana, huu ni utaratibu mzuri kwa sababu tunahitaji Taifa litakalounganisha masilahi ya pamoja.
Ushauri kwa wafanyabiashara
Katika hatua nyingine, Mbowe aliwashauri wafanyabiashara nchini kujiunga na vyama vya siasa vitakavyowapa fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ukiwamo ubunge, fursa aliyosema itawasaidia kufikisha ajenda na kero zao kwa ufanisi katika majukwaa husika.
Mbowe alitoa ushauri huo baada ya baadhi ya wafanyabiashara kutoa maoni yao wakitaka iwepo sheria itakayoruhusu mwakilishi wa jumuiya ya wafanyabiashara kuingia bungeni ili asaidie kujenga hoja na kuwasemea kero mbalimbali zinazowakabili.
Katika majibu yake, Mbowe alisema: “Sikilizeni wafanyabiashara, msisubiri kupewa viti maalumu, kwanza vinaleta ugomvi mkubwa kwa kina mama, ingieni kwenye vyama. Ingieni mkapambane kwa kuomba kura kwa wananchi na mtachaguliwa kupitia vyama hivyo.
“Mkifika Bungeni mtazungumza ajenda za biashara, Chadema kuna nafasi, kama mpo tayari jichagueni watu wenye sifa na makini tuwape majimbo muwanie”.
Alisema wakifika kwenye majimbo waombe kura kwa wananchi na wakiwachagua wajenge hoja.
“Hivi ndivyo wafanyabiashara wa Kenya wanavyofanya,” aliongeza.
Katika mkutano huo, baadhi ya wafanyabiashara waliacha kwa muda shughuli zao na kufuatilia hotuba ya Mbowe, naye akatumia nafasi hiyo kuwakaribisha Chadema akisema milango ipo wazi si kwa ubunge tu, bali hata nafasi nyingine za uongozi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.