TANGU akiwa mdogo Hamisa Mobetto anakiri alipenda sana kuwa mwanamuziki ila kutokana na kutafuta fedha akajikuta ameingia kwenye filamu na mitindo ambapo amepata mafanikio makubwa hadi kushinda tuzo kabla ya kuingia kwenye muziki.
Huyu ni Miss XXL After School Bash (2010), ni mshindi wa pili wa Miss Dar Indian Ocean (2011), pia aliwahi kuingia nusu fainali ya Miss Tanzania (2011) na 10 bora ya Miss University Africa (2012). Je, upande wa muziki yupo vipi? Bongo Music Facts inakudadavulia;
1. Katika wimbo wa Diamond Platnumz uitwao Nikifa Kesho kuna sauti ya Hamisa Mobetto ingawa hajatajwa kushiriki, hiyo ni sawa na Nandy na Ruby katika wimbo wa Christian Bella, Ollah.
2. Urafiki wa Hamisa Mobetto na Lira Garole ulianzia kwenye mtandao wa Instagram kwa kutumia Direct Message (DM). Lira aliwahi kuwa mpenzi wa msanii toka Marekani, Chris Brown, pia alionekana kwenye video ya wimbo wa Rick Ross na Chris Brown, Sorry.
3. Wimbo wa Hamisa, Madam Hero umeandikwa na msanii Foby na Prodyuza C 9. Utakumbuka Foby ndiye amehusika kwenye kuandika na kutunga melody za wimbo wa Dayna Nyange, Komela.
4. Sauti ya kike inayosikika kwenye wimbo ‘Jibebe’ wake Diamond Platnumz, Lava Lava na Mbosso ni yake Hamisa. Yaani yule anayeitikia ‘I like’ ni Hamisa. Huu unakuwa wimbo wa pili wa Diamond ambao Hamisa kaingiza sauti (back vocal) bila kutajwa kama amehusika.
5. Wengi wanajua kuwa wimbo wa kwanza Hamisa Mobetto kurekodi ni Madam Hero kutokana na kuwa ndio wa kwanza kuachiwa toka kwake. Hata hivyo Hamisa alianza kurekodi wimbo uitwao Furaha bado haujatoka hadi sasa.
6. Mwaka 2021 Hamisa alitambulisha lebo yake, Mobetto Music na kuwa msanii wa pili wa kike Bongo kutumia jina la familia upande wa lebo, wa kwanza ni Vanessa Mdee ambaye lebo yake ameipa jina la Mdee Music.
7. Hamisa alikuwepo wakati Tanasha anashuti video ya wimbo wa Alikiba, Nagharamia. Ikumbukwe Tanasha na Hamisa wamezaa na Diamond, lakini wakati huo wote bado walikuwa hawana mahusiano na Diamond.
8. Hamisa ndiye msanii wa kike kutoka kwenye Bongofleva anayeongoza kuwa na wafuasi (followers) wengi Instagram akiwa nao zaidi milioni 9.3 akiwa amempita Shilole ambaye sasa anashika nafasi ya pili akiwa na milioni 9.
9. Hamisa ni shabiki mkubwa wa Mwana FA na wimbo alioanza kuupenda kutoka kwa rapa huyo unaitwa Kama Zamani uliotoka Mei 2013 akiwashirikisha Kilimanjaro Band (Njenje), Mandojo na Domo Kaya.
10. Ili Hamisa aweze kutokea kwenye video ya msanii ni lazima yeye ndiye awe mhusika mkuu (main character). Utakumbuka tayari ametokea kwenye video kama Dodo ya Alikiba ambayo hadi anafika Zanzibar kwa ajili ya kushuti hakujua kama Hamisa atatokea kwenye video hiyo, ni jambo lililopangwa na uongozi wa Kings Music.