Dodoma. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dk Tulia Akson amemwapisha Mbunge wa kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha kushika wadhifa huo leo Aprili 5 jijini Dodoma.
Nahodha ameapishwa kuwa mbunge kufuatia uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan aliofanya hivi karibuni baada ya aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Hii ni mara ya pili kwa Nahodha kuteuliwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambapo awali ilikuwa ni katika kipindi cha awamu ya nne ambapo aliyekuwa Rais wa awamu hiyo, Jakaya Kikwete alimteua na kisha akampa Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi.
Uteuzi wa Nahodha aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unahitimisha nafasi 10 alizonazo Rais Samia kwa mujibu wa sheria.
Mbunge huyo alipomaliza kiapo chake, kama ilivyo kwa taratibu za kibunge, aliwasalimia baadhi ya wabunge na Waziri Mkuu kisha akaongozwa moja kwenye kiti ambacho kilikuwa kikitumiwa na Polepole.
Mwananchi