Jacqueline Mengi Mjane wa Dk Mengi Apata Ushindi Rufaa ya Mirathi

 

Jacqueline Mengi Mjane wa Dk Mengi Apata Ushindi Rufaa ya Mirathi

Dar es Salaam. Jacqueline Ntuyabaliwe ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, marehemu Reginald Mengi, ameshinda pingamizi alilowekewa na wasimamizi wa mirathi katika rufaa ya mirathi.

Ameshinda pingamizi hilo baada ya Mahakama kukataa hoja zote saba za pingamizi la wasimamizi wa mirathi.

Hii ni mara ya pili kwa mjane huyo kushinda pingamizi kutoka kwa wasimamizi wa mirathi hiyo wanaopinga kusikilizwa maombi yake ya mapitio.

Jacqueline na wanawe, Jaden Mengi ambaye ni mwombaji wa pili na Ryan Mengi (mwombaji wa tatu), wamefungua maombi ya mapitio katika Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu iliyobatilisha wosia wa marehemu Mengi.

Hata hivyo, wasimamizi wa mirathi hiyo, Abdiel Mengi (mtoto wa marehemu Mengi wa mke wa kwanza na Benjamin Abrahamu Mengi, ndugu wa marehemu Mengi), wanazuia rufaa yake hiyo isisikilizwe na yatupiliwe mbali.

Awali, baada ya Jacqueline kufungua maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu, wasimamizi hao walimwekea pingamizi wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali mapitio kwa madai yalikuwa yamewasilishwa isivyo halali.

Wasimamizi walidai kuwa, waombaji walipaswa kukata rufaa na sio kuwasilisha maombi ya mapitio waliyodai yalikuwa na upungufu wa kisheria kwa kutoambatanishwa nyaraka muhimu.

Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ilitupilia mbali hoja za pingamizi la kina Abdiel, badala yake ikakubaliana na hoja za Jacqueline zilizotolewa na wakili wake, Audax Kahendaguza na ikakubali kumsikiliza katika maombi yake hayo ya mapitio.

Kutokana na uamuzi huo, kina Abdiel wakawasilisha maombi ya marejeo wakiiomba Mahakama irejee na kubadilisha uamuzi wake wa kutupilia pingamizi lao dhidi ya maombi ya mapitio ya Jacqueline na wanaye. Katika maombi hayo, kina Abdiel walidai kuwa uamuzi wa Mahakama hiyo haukuzingatia misingi ya kisheria.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wa Jacqueline, Kahendaguza na wakili wa wajibu maombi wengine, waliotajwa kwenye wosia huo, walipinga hoja za kina Abdiel.

Mahakama ya Rufani juzi, ilikataa hoja zote za maombi ya marejeo ya kina Abdiel. Mahakama hiyo itasikiliza maombi ya mapitio ya Jacqueline na wanaye kwa tarehe itakayopangwa na Msajili wa Mahakama hiyo, ambayo ndiyo itatoa hatima ya uhalali wa wosia huo na uhalali wa Abdiel na Benjamin kuwa wasimamizi wa mirathi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad