Maunda Zorro imebaki historia. Mwili wake tayari umezingirwa na udongo ndani ya kaburi. Hatunaye kinafsi na kimwili pia. Mungu Mwenyezi wetu amuepushe na adhabu ya kaburi.
Aliishi na watu vizuri, ndo maana taarifa za kifo chake zilishitua wengi. Pengine kuliko hata ujio wa nyimbo zake mpya miaka kadhaa nyuma. Yes! Wasanii na Wabongo wengi wameumizwa sana na kifo cha Maunda.
Sauti, macho, utulivu na lugha zake za Kiswahili fasaha na kiingereza amazing. Vilimfanya awe wa pekee sana kisanii. Kifo chake pia kimetupa picha kamili kuwa alikuwa na watu na alikuwa mtu wa watu.
Ili ujue hilo, kafariki akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea msibani kwa rafiki yake. Hata mashuhuda wengi wa kabla ya umauti wake, maelezo yao yanakupa picha, kuwa alikuwa mtu wa watu.
Lakini aina ya kifo chake (ajali), kinatoa picha gani kwetu na wasanii wetu? Kifo ni kifo tu, na wakati wa Mungu ukifika hauna kinga. Lakini haituzuii kutazama kifo cha Maunda kama somo kwetu.
James Dandu 'Mtoto wa Dandu', ajali ya gari. Complex na Vivie, ajali ya gari. Sharomilionea ajali ya gari, kundi la taarabu la 5 Stars kina Issa Kijoti, ajali ya gari. Wote wameondoka kwa ajali za magari wakiwa vijana wadogo sana.
Ukiachana na kizazi kipya, 2 January, 1979 mpiga gitaa, muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi Mbaraka Mwishehe. Alifia hospitalini Mombasa nchini Kenya, muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari. Naye pia alifariki akiwa na miaka 34 tu.
Christina Joseph Lucas
Insta: @officialtinana .