Mwanza. Zikiwa zimeshatimia siku tano tangu mhubiri Diana Bundala, maarufu ‘Mfalme Zumaridi’ akamatwe na aendelee kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa mahojiano kuhusu tuhuma kadhaa, ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, kaka wa mhubiri huyo, Ernest Bundala alisema kadi za benki (ATM)ndugu yake zimechukuliwa na polisi
Akizungumza na Mwananchi, mara baada ya kuwapo kwa taarifa za askari polisi kuvamia tena nyumbani kwa dada yake, Ernest alisema askari hao walitaka wakabidhiwe kadi za benki lakini hawakupata ushirikiano walioutaka na kuwatia mbaroni watu wengine wanne, wakiwemo watoto wawili wa mhubiri huyo ambao hata hivyo waliachiwa baadaye.
“Baada ya kuona hawapati ushirikiano, polisi hao waliondoka na watoto wawili wa ‘Mfalme Zumaridi’, ndugu mmoja na muumini waliyemkuta hapa. Waliwaachia baada ya kupata kadi moja ya benki,” alisema Ernest.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Kamanda Ng’anzi alisema wanaendelea na uchunguzi
“Polisi tunaendelea kukusanya ushahidi wa kuwezesha watuhumiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote. Hilo la polisi kuwakamata watu wengine nyumbani kwa Zumaridi hakuna,” alisema Kamanda Ng’anzi
Februari 26, mwaka huu, ‘Mfalme Zumaridi’ na waumini 149, wakiwemo watoto 24 waliokutwa nyumbani kwake eneo la Bugugu Kata ya Mkolani jijini Mwanza walikamatwa na polisi na wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano.
Maisha kama kawaida
Hali na mfumo wa maisha nyumbani kwa mhubiri huyo yameendelea kama kawaida kwa ndugu, jamaa, marafiki na waumini kuendelea na shughuli zao za kila siku huku ulinzi ukiwa umeimarishwa na kikosi chake maalumu cha ulinzi maarufu kama askari wa Makerubi na Maserafi.
“Sisi tunaendelea na maisha kama kawaida huku tukifanya maombi maalumu kuwezesha “Mfalme Zumaridi’ na wengine wanaoshikiliwa kuachiwa huru. Ikulu ya ‘mfalme’ haijazingirwa wala kuwekewa ulinzi wa polisi. Tunasikia watu wakidai eti hakuna anayeruhusiwa kuingia humu; siyo kweli kwa sababu tunaingia na kutoka bila tatizo lolote,” alisema mmoja wa waumini aliyekutwa nje ya uzio nyumbani kwa Zumaridi
Nyumba yake
Wafuasi wa mhubiri huyo wanaona eneo ambalo nyumba ya kiongozi wao ipo ni patakatifu na wanapaita Ikulu ya mfalme’.
Pamoja na kuzungushiwa ukuta wa matofali unaokadiriwa kuwa na urefu wa futi sita kwenda juu, ‘ngome au ikulu’ ya “Mfalme Zumaridi’ ina ulinzi wa vijana wake maarufu kama ‘askari Makerubi na Maserafi’ wanaovaa mavazi maalumu na miwani mieusi muda wote ambao humhoji mtu yeyote asiyefahamika kabla ya kumruhusu kuingia ndani.
Ukuta wa ngome hiyo umepambwa kwa nakshi za aina mbalimbali ikiwemo maua na picha za aina tofauti ikiwemo yenye taswira ya simba dume huku kukiwa na maandishi yanayosomeka “Mfalme wa wafalme Zumaridi’’
Kwa jicho la haraka, Mwananchi ilishuhudia nyumba nne za kisasa zikiwa ndani ya ngome hiyo iliyojengwa katika eneo linalokadiriwa kuwa na urefu wa hatua 100 na upana wa hatua 50.
‘Mfalme Zumaridi', waumini wapandishwa kizimbani, wakataa dhamana
Diana Bundala maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi' na wenzake 92 leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mwanza wakikabiliwa na kesi tatu ikiwamo ya usafirishaji haramu wa binadamu. Soma zaidi