KOCHA msaidizi wa zamani wa Klabu ya Al Ahly ya nchini Misri, Cavin Johnson amesema kwamba, timu ya Orlando Pirates itakabiliwa na wakati mgumu mno itakapocheza na Simba wenye hatua ya robo fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, CAF, huku kwa mara ya kwanza Tanzania itatumia VAR kwenye Uwanja ....
wa Benjamin Mkapa na mashabiki 60,000 wameruhusiwa kuchuhudia.
Simba imepangwa kucheza na Pirates kwenye hatua hiyo baada ya kuitoa US Gendamarie ya Niger kwa ushindi wa 4-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Kwenye mchezo huu mwamuzi wa kati atakuwa ni Haythem Guirat kutoka Tunisia, akisaidiwa na mwamuziki msaidizi namba moja, Khalil Hassani (Tunisia), mwamuzi namba mbili Samuel Pwadutakam (Nigeria) na mwamuzi wa akiba ni Sadok Selmi (Tunisia).
Mwamuzi wa teknolojia ya usaidizi kwa njia ya video (VAR) atakuwa ni Ahmed Alghandour (Misri) na msaidizi wake ni Youssef Elbosaty (Misri) na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuitumia.
Katika mkutano wake na waaandishi wa habari wa Afrika Kusini, Johnson amesema itakuwa vigumu sana kwa Pirates na sio kitu rahisi kwao baada ya kupangwa na Simba kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
“Simba ni timu nzuri na inayosafiri sana, ina uzoefu wa kutosha na ni timu kubwa sana Tanzania,” alisema Johnson akiwaambia wanahabari.
“Kuikabili Simba nyumbani kwao ni ngumu sana, sijui ni watu elfu ngapi watakuwepo uwanjani kuwashuhudia.
“Lakini mara ya mwisho nilikuwa pale na Al Ahly kulikuwa na mashabiki 30,000 hadi 40,000 uwanjani, hivyo utakuwa mchezo mgumu sana kwa Pirates nchini Tanzania na wanatakiwa kujiandaa vilivyo kuwakabili,” aliongeza kocha huyo.
Simba iliichapa Al Ahly bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ikiwa chini ya Kocha Mkuu wa sasa raia wa Afrika Kusini Pitso Mosimane akisaidiwa na Johnson kwenye mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Februari 23, 2021.
Lilikuwa ni bao la raia wa Msumbiji, Luis Miquissone, ambalo lilimpa moja kwa moja tiketi ya kusajiliwa na klabu hiyo ambao ni Mabingwa wa Afrika kwa sasa.
Ulikuwa ni msimu ambao Simba iliongoza kundi A, ikiwa na pointi 13, ikifuatia na Al Ahly ambayo ilimaliza ikiwa na pointi 11, AS Vita Club ya Jamhuri ya Kimokrasi ya Congo pointi saba na Al Merrikh ya Sudan iliyomaliza na pointi mbili.
Johnson mwenye umri wa miaka 63 raia wa Afrika Kusini, amewahi pia kuwa kocha mkuu wa timu za Platinum Stars (mara mbili), SuperSport United, AmaZulu na Black Leopards (zote za Afrika Kusini).
Oktoba mwaka 2020, aliteuliwa kwa kocha msaidizi wa Al Ahly chini ya Pitso Mosimane ambako alidumu hadi mwaka 2021.
Simba itaanzia nyumbani Aprili 17, kabla ya kusafiri kwenda Houghton Jijini Johannesburg kwa mchezo wa marudiano Aprili 24.