Kuabudiwa Kwa Mtu na Matokeo yake



FEBRUARI 25, 1956, Katibu Mkuu wa Chama cha Komunisti, Nikita Krushchev, alitoa hotuba maarufu iliyoitwa “The Personality Cult and Its Consequences” – “Kuabudu Mtu na Matokeo Yake". Pia huitwa “Hotuba ya Siri.”

Ukumbi wa Great Kremlin, Moscow, Urusi, ukiwa na jopo la wajumbe 1,500 kutoka nchi za Umoja wa Sovieti, pamoja na mamia ya wageni waalikwa, walinyamaza kimya kwa dakika 240, wakimsikiliza Krushchev akitema nyongo.

Sio tu kwamba wajumbe na wageni waalikwa walinyamaza, bali pia walishindwa hata kugeuza shingo kutazamana wao kwa wao. Wote macho yao yalikuwa pima kumtazama Krushchev, kwa hofu kubwa. Krushchev aliamua kuvaa mabomu kuusema ukweli ulioogopwa na wengi.

Krushchev alitoa hotuba hiyo ikiwa ni miaka mitatu kasoro siku tisa tangu kifo cha aliyekuwa Mtawala wa Sovieti, Joseph Stalin kilichotokea Machi 5, 1953. Tangu kufa kwa Stalin, hakuna lolote baya lililotamkwa kuhusu kiongozi huyo ndani ya Sovieti.

Viongozi waliofuata baada ya Stalin, walipitia kipindi kigumu kwa kila walichofanya. Maana walipimwa kwa utendaji wa Stalin. Ndani ya Urusi na Sovieti yote, Stalin alitukuzwa mithili ya Mungu mtu.

Krushchev alisema, Stalin aliua watu wengi, wapinzani wake, watiifu wa chama pamoja na kutekeleza unyama mwingine wa kila aina, na hayo ni matokeo ya kumtukuza mno na kumwabudu kama Mungu.

Baada ya hapo, Krushchev alimtangaza Stalin kama mtu mwovu. Kumbukumbu mbalimbali za Stalin zilianza kuondolewa. Stalin alipokufa mwili wake haukuzikwa, ulihifadhiwa jirani na Kiongozi wa zamani Sovieti na Chama cha Komunisti, Vladimir Lenin, ndani ya jumba la Makumbusho la Lenin.

Mwaka 1961, katika kuhakikisha kumbukumbu za Stalin zinafutwa, mwili wake uliondolewa kwenye Jumba la Makumbusho la Lenin, ukazikwa makaburi ya Kremlin Wall kama mtu wa kawaida.

SOMO: Madikteta huwa na sumu ya ajabu sana kwa umma. Hutokea kupendwa na kuabudiwa licha ya kufanya unyama mwingi. Kuna wanaomuenzi Mobutu Sese Seko, wapo wanaosema Idi Amin alikuwa kiongozi mzuri. Hata Adolf Hitler anaenziwa. Katika utawala wake, Stalin anahusishwa moja kwa moja na vifo vya watu wanaofikia 20 milioni.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad