Kwa Viungo Hawa Kazi kwa Mkapa..Hatoki Mtu Leo



MBINU ya kutumia idadi kubwa ya wachezaji katikati mwa uwanja huenda ikaongeza utamu wa mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba itakayochezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni.

Kama ambavyo makocha wa timu hizo mbili wamekuwa wakifanya katika mechi nyingi za nyuma ambazo Yanga na Simba zimecheza katika mashindano tofauti ambapo zilikuwa zikitumia namba kubwa ya wachezaji katika safu ya kiungo, ndivyo inavyotarajiwa katika mechi ya kesho.

Yanga inayonolewa na kocha Nasreddine Nabi, imekuwa ikitumia zaidi mfumo wa 4-2-3-1 kama ambavyo mwenzake wa Simba, Pablo Franco amekuwa akifanya hivyo katika mechi zao mbalimbali.

Mwanaspoti linajaribu kuvuta taswira ya namna viungo wa timu zote mbili watakavyopambana katikati mwa uwanja kesho katika harakati za kusaidia timu zao kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.


Saido v Kanoute

Katika mechi sita za Ligi Kuu zilizopita, Saido Ntibazonkiza amehusika na mabao matatu akifunga mawili na kupiga pasi moja ya mwisho na amekuwa na kiwango bora msimu huu.

Safari hii anakwenda kukutana na Sadio Kanoute wa Simba ambaye ana uwezo mkubwa wa kupora mipira na kuichezesha timu.

Fei Toto v Mkude

Jonas Mkude kwa sasa ndiye mchezaji aliyecheza idadi kubwa ya mechi za dabi ya Kariakoo kwani ameitumikia Simba kwa muda wa miaka 11 sasa.


Uwezo wake wa kuilinda safu ya ulinzi, kuchezesha timu na kupiga pasi zinazofikia walengwa kwa usahihi utakutana na kipimo kigumu cha kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ana uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kufunga mabao kwa mashuti ya mbali.

Chama v Bangala

Tangu alipojiunga na Yanga, Yannick Bangala amejitambulisha kama mmoja wa viungo bora wa ulinzi wa Yanga na uwepo wake umechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya timu hiyo kuruhusu mabao sita tu kwenye nyavu zake.

Hata hivyo, kesho atakuwa na shughuli pevu mbele ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama ambaye ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao na katika mechi sita zilizopita za Ligi Kuu, amefunga mabao matatu.

Sakho v Aucho

Kasi, chenga na uamuzi wa haraka pindi awapo na mpira mguuni, ni sifa ambazo zimemfanya Pape Osmane Sakho kuwa mchezaji muhimu na tegemeo katika kikosi cha Simba.


Lakini shughuli ya kumkabili Sakho itaongozwa na kiungo Khalid Aucho ambaye anasifika kwa uwezo mkubwa wa kuichezesha timu, kuziba mianya na kutibua mipango ya viungo wa timu pinzani katikati akichagizwa na utulivu wake pindi awapo na mpira au hata asipokuwa nao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad