Lissu amshauri Rais Samia ang’oe vigogo wa awamu ya tano



MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan, awaondoe madarakani viongozi wa umma hasa wa vyombo vya ulinzi na usalama, waliowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Hayati John Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Lissu ametoa ushauri huo jana jioni, katika mjadala uliofanyika mtandaoni, kuhusu utata wa kukamatwa kwa Wakili Peter Madeleka.

Mwanasiasa huyo amedai kuwa, kitendo cha Wakili Madeleka kukamatwa katika mazingira ya utata, kinakinzana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa hivi karibuni katika ziara yake nchini Marekani, kwamba anataka kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kidemokrasia.

“Rais Samia yuko Marekani wiki nzima, ametoa ahadi kubwa kwamba Serikali yake hataki kuwa kama Magufuli, amezungumza nje na tumesikia. Sasa wakati Rais hata wino alioandika kauli zake haujakauka kwamba atahakikisha tunarudi kuwa nchi ya kidemokrasia, jeshi lake linamkanusha hadharani,” amesema Lissu.


 

Lissu amesema “nimwambie Rais atue mizigo mizito ya Magufuli, hii ni mizigo. Kama Rais anataka kauli zake zichukuliwe kwa uzito tumwambie atue haya magunia mazito sababu wakiendelea kubaki watamharibia urais wake.”

Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema Bara, amekishauri Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kiendelee kupaza sauti ili mwanachama wake Madeleka aachwe huru na Polisi.

“Nimesikia Rais wa TLS (Prof. Edward Hoseah)ameingilia kati haya masuala ambayo chama chake imekuwa kimya sana kwa miaka mingi kwenye matukio kama haya,” amesema Lissu.


Madeleka alikamatwa na Jeshi la Polisi mchana wa tarehe 20 Aprili 2022, akiwa kwenye maegesho ya magari ya Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Wakili Abdullah Lyana, amesema Rais wa TLS, Profesa Edward Hoseah, amewasiliana na viongozi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya suala hilo na kwamba Wakili Madeleka, aliyeko mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, atatoka muda wowote baada ya kukamilisha taratibu za dhamana.

Mwanahalisi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad