Majanga yaendelea kuikumba Ukraine



 
Lyiv, Ukraine. Mfululizo wa mashambulizi ya nguvu ya Russia dhidi ya miundombinu ya kijeshi huko Lviv, Ukraine, yamesababisha vifo vya watu kadhaa na mji wa magharibi mwa Ukraine kuwaka moto. Mji huo uliepushwa na mapigano makali hapo awali.

Mkazi wa Lviv aliliambia shirika la habari la AFP kwamba waliona moshi mwingi ukipanda juu ya majengo ya makazi na ving’ora vya mashambulizi ya anga vilisikika katika jiji lote wakati na baada ya shambulizi hilo.

“Kwa sasa, tunaweza kuthibitisha watu sita wamekufa na wanane wamejeruhiwa. Mtoto alikuwa miongoni mwa waathirika,” alisema gavana wa mkoa wa Lviv, Maksym Kozytsky kwenye mtandao wa kijamii.

Alisema makombora manne ya Russia yalilenga miundombinu ya kijeshi ya Ukraine na kituo cha matairi ya gari pia kilishambuliwa.


 
“Moto ulizimwa kutokana na mgomo huo. Bado unazimwa. Vifaa viliharibiwa vibaya,” alisema Kozytsky.

Andrei (21), mkazi wa Lviv alisema alikuwa amelala wakati ving’ora vikilia saa 2 asubuhi.

“Nililala wakati wa mashambulizi matatu ya kwanza, lakini la mwisho lilipopigwa ilikuwa kama madirisha yangu yalikuwa karibu kuvunjika na samani zikasogea,” aliiambia AFP.


Lviv, karibu na mpaka wa Ukraine na Poland, umeepushwa kuhusika katika mapigano mabaya zaidi yaliyosababishwa na uvamizi wa Urusi kwa jirani yake anayeunga mkono magharibi karibu miezi miwili iliyopita.

Mji huo badala yake umekuwa kimbilio la watu waliokimbia makazi yao kutoka mashariki iliyokumbwa na vita na mwanzoni mwa mapigano ulihifadhi balozi kadhaa za magharibi zilizohamishwa kutoka Kyiv.

Mashambulizi hayo yalitokea jana wakati Russia ikizidisha mashambulizi ndani na karibu na mji mkuu wa Kyiv mashariki zaidi, yakilenga kwa siku kadhaa vituo kadhaa vinavyotengeneza vifaa vya kijeshi.

Mashambulio hayo yanatokea baada ya Russia kuapa kuongeza mashambulizi katika mji mkuu kujibu kile maofisa wa jeshi la Russia walidai kuwa ni mashambulizi ya Ukraine katika ardhi ya Russia na kuzama kwa meli ya kivita ya Moskva.


 
“Makombora matano yenye nguvu yanashambulia mara moja miundombinu ya kiraia ya mji wa kale wa Ulaya wa Lviv,” msaidizi wa Rais wa Ukraine, Mykhaylo Podolyak aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

“Warusi wanaendelea kushambulia kwa ukatili miji ya Ukraine kutoka angani, wakitangaza kwa dunia nzima ‘haki’ yao ya kuua raia wa Ukraine,” alisema.

Mkuu wa shirika la reli la kitaifa la Ukraine, Alexander Kamyshin alisema kwenye mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya miundombinu ya tovuti hiyo imeharibiwa na kuna uwezekano kungekuwa na ucheleweshaji wa huduma, lakini hakuna abiria au wafanyakazi waliojeruhiwa.

Waandishi wa habari wa AFP waliona moshi mweusi ukifuka kutoka kwa paa lililoharibika la karakana ya kutengeneza magari juu ya njia za reli kaskazini magharibi mwa jiji, karibu kilomita nne (maili 2.5) kutoka katikati ya jiji.


Lviv, mwishoni mwa Machi ilikumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya Russia ambayo yalilenga ghala la mafuta na kuwajeruhi watu watano. Machi 18, milipuko ya mabomu iligonga kiwanda cha kutengeneza ndege karibu na uwanja wa ndege wa Lviv. Hakuna majeraha yaliyoripotiwa.

Wakati mashambulizi hayo yakitekelezwa, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky aliishutumu Russia kutaka kuharibu eneo lote la mashariki la Donbas, kwani vikosi vya mwisho vilivyosalia katika bandari ya kimkakati ya Mariupol vilijiandaa kwa utetezi wa mwisho.

Russia inashinikiza kupata ushindi mkubwa katika mji huo wa kusini huku ikijitahidi kupata udhibiti wa Donbas na kutengeneza ukanda wa ardhini kuelekea Crimea ambayo tayari imechukuliwa.

Hata hivyo, Ukraine imeahidi kuupigania na kuulinda mji huo, ikikaidi kauli ya Russia Jumapili iliyowataka wapiganaji waliosalia ndani ya kiwanda cha chuma cha Azovstal kuweka silaha chini na kujisalimisha.

Mamlaka ya Ukraine imewataka watu mjini Donbas kuhamia magharibi, ili kuepuka mashambulizi makubwa ya Russia kwa lengo la kukamata maeneo ya Donetsk na Lugansk.


 
“Wanajeshi wa Russia wanajiandaa kwa operesheni ya kikatili mashariki mwa nchi yetu katika siku za usoni. Wanataka kumaliza kihalisi na kuiangamiza Donbas,” alisema Zelensky katika taarifa ya jioni.

Mariupol imekuwa ishara ya upinzani mkali wa Ukraine ambao haukutarajiwa tangu wanajeshi wa Russia walipovamia jimbo la zamani la Soviet Februari 24. “Jiji bado halijaanguka,” Waziri Mkuu, Denys Shmyhal alisema. “Bado kuna vikosi vyetu vya kijeshi, wanajeshi wetu. Kwa hivyo watapigana hadi mwisho,” aliambia ABC wiki hii.

Hatutajisalimisha

Wakati miji mikubwa kadhaa ikiwa imezingirwa, alisema hakuna hata mmoja isipokuwa Kherson kusini ilioanguka na zaidi ya majiji na miji 900 ilikuwa imetekwa tena.

Gavana wa Lugansk Sergiy Gaiday alisema wiki ijayo itakuwa ngumu.

“Huenda ikawa mara ya mwisho tunapata nafasi ya kukuokoa,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Vikosi vya Russia viliendelea kushambulia eneo la mashariki la Lugansk na watu wawili walikufa katika mji wa Zolote, aliambia vyombo vya habari vya Ukraine mapema siku hiyo.

Na mashambulizi matano ya nguvu ya makombora ya Russia yalipiga mji wa Lviv mapema jana, katika shambulio la nadra katika mji wa magharibi ambao hadi sasa umekingwa na mapigano mengi tangu uvamizi huo uanze karibu miezi miwili iliyopita.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad