Baada ya majeshi ya Urusi kupunguza mapigano katika Miji ya Kyiv na Kharkiv taarifa zimeibuka juu ya mauaji ya kikatili na unyanyasaji wa kijinsia uliothibitishwa na Waziri Mkuu wa Ukraine kupitia ushahidi wa picha zilizopigwa na mashirika ya uangalizi wa haki za binadamu kwenye baadhi ya miji nje kidogo ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Jumla ya watu 410 wameuawa katika miji ya Bucha na Irpin magharibi mwa Jiji la Kyiv, miili mingi ya watu imeonekana pembezoni mwa barabara na mingine ikiwa imelundikwa katika mashimo.
Baadhi ya waandishi wa habari waliofanikiwa kubaki katika maeneo ambayo majeshi ya Urusi yameondoka baada ya kusimamisha mapigano, wamedai kuwa ushahidi wa wazi umeonekana unaoonesha utekelezaji wa makosa ya uhalifu wa kivita uliotekelezwa na majeshi hayo ikiwemo miili ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi nyuma ya kichwa huku wakiwa wamefungwa kamba mikononi lakini pia miili mingine ikiwa na alama za michubuko ya mateso pamoja na kubakwa.
Baadhi ya miili ya raia wa Ukraine iliyotelekezwa ikibebwa kwa ajili ya mazishi
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amewaongoza viongozi wa nchi Duniani kukemea vitendo vya kikatili na anavyoviita vya uhalifu wa kivita na ameahidi kutoa misaada kwa Ukraine lakini pia kutoa timu ya wataalamu wa uchunguzi kwenda Mahakama ya Uhalifu wa Kivita The Hague ili kusaidia ukusanyaji wa ushahidi wa matukio ya uhalifu wa kivita.
Katika Moja ya kauli zake Waziri Mkuu Johnson alisema:
“Hatuwezi kupumzika hadi pale haki itakapotendeka.”
Muonekano wa baadhi ya miili ya watu waliofariki katika mji wa Bucha nje kidogo ya Jiji la Kyiv
Kwa upande mwingine Tymofiy Mylovanov mshauri wa rais wa Ukraine na Waziri wa zamani wa Fedha amesema kuna uwezekano matukio makubwa zaidi yakawa yamefanyika katika miji mingine nje ya Jiji la Kyiv, lakini pia katika vitongoji mbalimbali kwenye Jiji la Kharkiv na hivyo kuwaomba waandishi wa habari na wanasheria kutembelea maeneo hayo na kuchukua kumbukumbu zote pamoja na taarifa muhimu zitakazothibitisha utekelezaji wa makosa ya uhalifu wa kivita.