KUELEKEA kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, makocha wa pande mbili Pablo Franco na Fadlu Davis, wameonekana 'kufanyiana umafia' kila mmoja akidai kunasa taarifa na mipango ya mwenzake.
Kocha Mkuu wa Simba, Franco amesema kuwa ilikuwa ni rahisi kwao kunasa taarifa na kuwapeleleza wapinzani wao kutokana na kuwa ni timu kubwa ambayo taarifa zao ziko wazi, lakini pia ana baadhi ya watu wa benchi la ufundi ambao wameshawahi kufanya kazi nchini humo, hivyo kuifahamu timu hiyo na Ligi ya Afrika Kusini kwa ujumla.
"Itakuwa ni mechi ya kimbinu, nimewafundisha wachezaji wangu jinsi ya kuitumia VAR, wanatakiwa kuwa makini kutofanya makosa, lakini wanatakiwa kucheza mpaka mwisho wa tukio, bila kuhofu kuwa filimbi itapigwa au la.
Nimewaambia wacheze mpaka wasikie filimbi, kwa sababu unaweza ukauacha mpira kumbe wala hujaotea. Ni kwamba VAR ndiyo itaamua, kwani unaweza kujiona labda umeotea, ukafunga bao, kumbe VAR itaonyesha hukuwa umeotea, au ukaacha, kumbe hukuwa umeotea, nimezungumza nao kuhusu hilo," alisema kocha Pablo na kuongeza.
"Nina kocha hapa wa makipa ameshawahi kuzifundisha timu za huko, kwa hiyo anaijua Orlando Pirates na ligi ya huko, nina mchezaji ambaye ameshacheza huko (Bernard Morrison), pia nina watu wanaokusanya taarifa, lakini ile ni timu kubwa ambayo wala hupati tabu sana kuifuatilia, kujua inatumia mfumo gani, wachezaji gani wa kuchungwa, kwa sababu inaweka sana taarifa zake kwenye mitandao ya kijamii, kwa hiyo ni rahisi kujua mbinu zake na nini tunatakiwa tufanye," alisema Pablo.
Taarifa za ndani za klabu hiyo zinasema kuwa kocha huyo alikabidhiwa na viongozi wa Simba video tatu za Orlando Pirates ambazo imecheza hivi karibuni kwa ajili ya kuzifanyia kazi, ambazo ni dhidi ya JS Saoura ya Algeria, Al Hittihad ya Libya ambazo ni za Kombe la Shirikisho na moja ya mechi ya Ligi Kuu Afrika Kusini ya hivi karibuni.
Kocha Msaidizi wa Orlando Pirates, Davis, akihojiwa na vyombo vya habari nchini humo, kabla ya kuanza safari alisema wanakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya timu inayotumia vema uwanja wake wa nyumbani, lakini imejipanga na wameifuatilia timu hiyo na kujua maeneo ambayo wana nguvu na mapungufu.
"Tunakwenda kukurana na timu nzuri. Timu inapocheza hatua hii ni lazima uipe heshima yake. Tunakwenda kucheza nyumbani kwao huku tukichukua tahadhari kubwa kwani wanapocheza kwao wanakuwa ni hatari zaidi. Simba wana washambuliaji wenye kasi, hatutakiwi kufanya makosa, hivyo tumeyafanyia kazi mapungufu yao, nguvu yao ilipo, kwani hatutakiwi kufanya makosa mengi hatarishi," alisema kocha huyo.