Maofisa BoT wabainika kupiga Sh3.99 bilioni za noti chakavu



Dar es Salaam. Kukosa uadilifu na upungufu wa udhibiti ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kumesababisha hasara ya Sh3.99 bilioni kwa noti ambazo hazikuwa na vigezo vya kuwa chakavu kati ya Januari 2019 hadi Septemba 2019.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Serikali Kuu ilisema noti 399,392 zenye thamani ya Sh3.99 bilioni hazikuwa na vigezo vya kupewa noti mpya na zilipewa noti mpya kwa udanganyifu. Noti hizo ni zaidi ya asilimia 95 ya noti zote chakavu katika kipindi hicho.

“Katika kipindi hcha Januari 2019 hadi Septemba 2019, nilibaini BoT ilipokea noti za Sh4.17 bilioni ambazo ni noti 417,006 za Sh10,000 ambazo zilidaiwa kuwa ni chakavu, ili zibadilishwe na kutolewa noti mpya.

“Udanganyifu uliofanywa na maofisa wawili na watunza fedha wanne wa Benki Kuu,” ilieleza ripoti hiyo.


 
Ripoti iliendelea kuchanganua kuwa noti 1,427 zenye thamani ya Sh14.27 milioni zilikuwa safi na zilifaa, hivyo hazikuwa na sifa ya kuwa noti chakavu.

“Nilibaini kuwa noti 16,187 zenye thamani ya Sh161.87 milioni zilikidhi vigezo vya kurejeshwa Benki Kuu na kutolewa noti mpya,” ilisema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa asilimia 95 ya fedha zilibainika hazikuwa chakavu, wahusika walifanya udanganyifu kwa kukata noti safi 199,696 vipande vilivyotoa noti takribani 399,392 vyenye thamani ya Sh10,000 kila kimoja kuvibandika kwenye karatasi nyeupe kisha wakadai noti mpya.


Kutokana na ubadhirifu huo, Benki Kuu ilipata hasara ya Sh20.68 milioni ya kuchapisha na kutoa noti 199,696 zilizotumika katika udanganyifu huo.

Dosari nyingine iliyobainika ni kutokutunza daftari la wateja waliokuwa wanabadilisha fedha chakavu, hivyo CAG hakuwatambua wateja waliobadilisha fedha chakavu katika kipindi husika.

Licha ya kikwazo hicho, alisema “nilibaini wateja 24 walikuwa na mtindo wa kutembelea Benki Kuu mara kwa mara kwa ajili ya kufanya miamala ya noti chakavu, ambao wamehusishwa kushirikiana na wafanyakazi wa benki hiyo kutekeleza mpango huo.”

CAG alipendekeza Gavana wa BoT achukue hatua stahiki za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi waliohusika katika ubadhirifu huo na kuhakikisha kunakuwapo usimamizi madhubuti wa miamala yote ya noti chakavu zinazobadilishwa Benki Kuu na kwenye Benki zote za Biashara.


 
Ubadhirifu maofisa Uhamiaji KIA

Katika ripoti hiyo, CAG alieleza kuwa Serikali imepata hasara ya Sh2.42 bilioni kutokana na stika 21,208 za viza zinazodaiwa kughushiwa na kumbukumbu zake kufutwa kwa makusudi kwenye Mfumo wa Maombi ya Viza (VAS) na maofisa uhamiaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Ilielezwa kati ya Januari mosi 2019 hadi Juni 30, 2019 ukaguzi ulibaini Watanzania 41 na wageni 107,119 waliwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wageni 33,558 waliwasili kupitia KIA, ingawa taarifa zao ambazo ni pamoja na stakabadhi za mapokezi ya fedha (ERV), fomu za kuingia nchini, pamoja na taarifa za uwekaji fedha benki hazikuweza kupatikana.

Kutokana na sababu hiyo, ripoti hiyo ilieleza CAG hakujua ni kiasi gani cha mapato ambayo Serikali ilipaswa kupata kutoka kwa wageni hao.


“Katika uchunguzi zaidi, niligundua taarifa za stika 21,208 za viza za wageni waliowasili nchini kupitia KIA zilifutwa kutoka kwenye kanzidata ya mfumo wa ‘VAS’.

“Stika hizo zilizoondolewa ziliwahusu wageni ambao walipaswa kulipa viza walipowasili, lakini maofisa 32 wa Idara ya Uhamiaji KIA walifanya njama na kuwapatia wageni hao stika za viza za kughushi na kujipatia Sh2.42 bilioni kutoka kwao,” ilieleza ripoti hiyo.

Hivyo, alipendekeza Idara ya Uhamiaji ichukue hatua stahiki za kisheria na kinidhamu dhidi ya maofisa 32 wa idara hiyo kituo cha KIA ambao wanahusika kuisababishia Serikali hasara.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad