MASHABIKI wa Simba walikuwa na hamu kubwa ya kutaka kuona winga Bernard Morrison anaenda Sauzi kukinukisha kwenye mechi ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, lakini mambo yametibuka.
Wasauzi wamemkomalia winga huyo raia wa Ghana na kumzuia kutimba huko, licha ya mabosi wa Simba kupambana kwa karibu wiki nzima ili kuweka mambo sawa baada ya kubaini alikuwa na marufuku ya Idara ya Uhamiaji kuingia nchini humo.
Simba imepanga kuondoka kati Aprili 21 au 22 kwenda Sauzi kurudiana na Orlando katika mechi itakayopigwa Aprili 24, lakini Morrison hatakuwa kwenye msafara huo baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez kukiri wamekwama.
Barbara alisema rasmi jambo hilo limeshindikana kama ilivyokuwa msimu uliopita walipoenda kucheza na Kaizer Chiefs katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika naa kufungwa mabao 4-0.
Mtendaji huyo alisema taarifa za Morrison na ataenda huko sio za kweli.
“Tuliwasiliana na watu wa Mamlaka za Uhamiaji Afrika Kusini kuomba kupata ruhusa ya kuingia na Morrison, walitueleza sheria zao mtu akivunja hawezi kupata tena nafasi ya kuingia,” alisema Barbara na kuongeza;
“Wametuambia kutokana na kosa lake mamlaka haipo tayari kumruhusu kutokana na sheria zilivyo, hivyo ni rasmi sasa Morrison hatakwenda Afrika Kusini. Baada ya mechi dhidi ya Polisi Tanzania (iliyochezwa jana) tutamjulisha kocha ili afahamu hilo na kuona jinsi ya kujipanga kwa mechi ya ugenini bila ya Morrison.”
Barbara alisema wameongea na Morrison aliyefunga mabao smatatu na kuasisti nne katika michuano hiyo, kuwa kama ikitokea amepata nafasi ya kucheza hapa nyumbani apambane zaidi ili kuirahisisha kazi kwa mechi ya Sauzi.