Maskini...Watoto Wawili Wajinyonga kwa Kukaripiwa Utoro Shule



Watoto wawili katika Wilaya ya Kigoma na Uvinza mkoani Kigoma wamejinyonga kwa kile kinachoelezwa kukasirishwa na makaripio kutoka kwa wazazi wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, James Manyama akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini hapa jana alisema watoto hao ambao hawakuwa wakihudhuria masomo shule walifanya hivyo baada ya kukemewa na wazazi wanaopinga vitendo vya utoro shuleni vya watoto hao.

Alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea katika Kijiji cha Matyazo mkoani Kigoma wiki iliyopita baada ya Peter Philipo (14) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Luiche kujinyonga kwa kanga aliyoifunga kwenye kenchi za nyumba yao.

“Chanzo cha mtoto huyo kujinyonga ambaye alikuwa akiishi na bibi yake inaelezwa kuwa amekuwa na tabia ya kutohudhuria masomo tangu kufunguliwa shule mwezi Januari mwaka huu, lakini pia tabia za utukutu kwa bibi yake ndipo baba yake aliposikia hivyo alifika nyumbani alipokuwa akiishi marehemu na kumuadhibu na ndipo mtoto huyo akachukua maamuzi hayo,” alisema.


Aidha, katika tukio lingine lililotokea katika Kijiji cha Nguruka, Wilaya ya Uvinza Machi 28 mwaka huu, Kelvin Yosia (12) mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Nguruka alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila iliyokuwa ikitumika kuanikia nguo uani kwao.

Mtoto huyo aliyekuwa akiishi na bibi yake hakuwahi kuhudhuria shule tangu shule ilipofunguliwa mwaka huu na kwamba baba yake alitembelea kwa bibi yake na kupata habari hizo na kumuadhibu mtoto huyo kwa tabia hiyo na ndipo mtoto huyo akachukua hatua ya kujinyonga.

Katika hatua nyingine, Kamanda Manyama alisema kuwa polisi wamefanikiwa kukamata pikipiki moja aina ya King Lion iliyotelekezwa na watu wasiojulikana ambao walikimbia baada ya kuona uwepo wa polisi kwenye eneo wakidhaniwa kuwa walitaka kufanya tukio la ujambazi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad