Mataifa 18 yapeleka silaha vitani Ukraine



MATAIFA 18 yamesafirisha silaha za kivita nchini Ukraine, zikiwemo Amerika na Uingereza.

Baadhi ya silaha hizo ni makombora ya kulipua vifaru na ndege, droni, helikopta aina ya Mi-17 na bunduki.

Akihutubu jana kabla ya kikao rasmi cha mataifa wanachama wa Shirika la Kujihami (Nato) kuanza jijini Brussels, Ubelgiji, Waziri wa Mashauri wa Uingereza, Liz Truss, alisema kuwa Urusi inapaswa “kukabiliwa vilivyo”.

Alisema Urusi inafaa kuwekewa vikwazo vingi zaidi hadi pale itakapojiondoa Ukraine.


 
Akasema: “Muda wa kuendesha majadiliano na Urusi umeisha. Lazima tuanze mkakati mpya utakaohakikisha kuwa tumeizuia kuendelea kutekeleza ukatili dhidi ya raia nchini Ukraine.”

Kulingana na gazeti la The Times, wakuu wa kijeshi nchini Uingereza wanabuni mikakati ya kutuma magari ya kijeshi nchini Ukraine.

Lilisema Uingereza inaamini kuwa “wiki tatu zijazo zitakuwa muhimu kwenye maamuzi ya hatima ya uvamizi wa Urusi.”


Hilo lilijiri huku Ukraine ikiendelea kuyaomba mataifa zaidi kuisaidia kwa silaha.

Akihutubu jijini Brussels, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba alisema ombi kuu la Ukraine ni kusaidiwa kwa silaha ili kuikabili Urusi.

“Ajenda yangu ni: silaha, silaha na silaha,” akaeleza.

Mawaziri wa mashauri ya kigeni kutoka mataifa ya Nato walitarajiwa kuanza kikao maalum jijini humo, kujadili hali ya vita nchini Ukraine kuanzia leo Ijumaa.


 
“Jeshi letu na nchi nzima ya Ukraine imedhihirisha kuwa tunajua vita na hata kuwashinda wavamizi wetu. Hata hivyo, bila uwepo wa silaha za kutosha, itakuwa vigumu sana kuwashinda wavamizi hao,” akasema, kwenye kikao na wanahabari.

Akaongeza: “Ikiwa tutapata silaha hizo kwa haraka, hilo litatuwezesha kuwaokoa raia wengi. Hilo pia litatuwezesha kuvizuia vikosi hivyo dhidi ya kufanya uharibifu katika miji na vijiji vyetu kama mjini Bucha.”

Mataifa mengi duniani yamejitokeza kuikashifu Urusi kufuatia ukatili uliotekelezwa na vikosi vyake katika mji huo, ambao uko karibu na jiji kuu la Ukraine, Kyiv.

VIKWAZO

Mataifa ya Magharibi yametishia kuongeza vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya Urusi.


“Ninawaoma wanachama wa Nato kuondoa tashwishi yao dhidi yetu kuhusu ombi la kutupa usaidizi wa silaha. Ni ombi lenye uzito, japo hiyo ndiyo njia ya kipekee itakayotuwezesha kurejesha amani nchini mwetu,” akaeleza waziri huyo.

Alipuuzilia mbali mataifa yanayotilia shaka ombi hilo.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa wakipinga ombi la Ukraine kusaidiwa kwa silaha kama vifaru na ndege za kivita, akishikilia kuwa hilo “litakiuka kanuni za kimataifa kuhusu vita.”

Alisema huenda hilo likayaingiza mataifa hayo moja kwa moja kwenye vita hivyo.

Wakati huo huo, Austria jana iliziagiza mamlaka zake kuwafurusha wanadiplomasia wanne kutoka Urusi “kwa kuwa na mienendo ambayo hailingani na hadhi yao.”


 
Kulingana na msemaji wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Austria, wanadiplomasia hao wameagizwa kutoka nchini humo kufikia Jumanne wiki ijayo.

Wanadiplomasia watatu wanahudumu katika ubalozi wa Urusi jijini Vienna huku mmoja akihudumu katika jiji la Salzburg.

Hatua hiyo inajiri siku kadhaa baada ya mataifa kadhaa ya Ulaya kuwafurusha mabalozi wa Urusi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad