Mauigizaji maarufu wa filamu ya Ubelgiji Jean-Claude van Damme, anayejulikana pia kama Muscles kutoka Brussels, amefurahia kupewa pasipoti ya kidiplomasia ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo - na kusema kwamba analenga kuwashawishi nyota wengine kutembelea nchi hiyo.
"Nitajaribu kuwashawishi nyota wa kimataifa kama vile Stallone, Schwarzenegger, Jacky Chan na wengine wengi,"
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 61 alisema hayo mji mkuu, Kinshasa, alipokuwa akipokea hati yake ya kusafiria na jukumu lake kama balozi wa kitamaduni, vijana na wanyamapori.
"Pia kuna waimbaji kama Jennifer Lopez na wanasoka kama Messi, Ronaldinho, Cristiano Ronaldo. Ni lazima waje nchini ili kuonyesha kwamba iko salama, ili kuonyesha kwamba DRC inaweza kuwapa ulinzi watu maarufu”
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekabiliwa na miongo kadhaa ya kukosekana kwa utulivu, huku makundi mengi yenye silaha yangali yanarandaranda katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa nchi hiyo, yakiua, kubaka na uporaji.
Bingwa wa sanaa ya kijeshi, Van Damme aliendelea kuigiza katika filamu za kubwa za Hollywood kama vile Cyborg, Kickboxer na Universal Soldier - na hivi majuzi zaidi alionyesha Master Croc katika filamu za Kung Fu Panda.
Aliwashangaza watu katika mkutano na waandishi wa habari kwa kusema kwamba kweli alizaliwa DR Congo, akisema alikuwa "mzaliwa wa Likasi", jiji lililo kusini-mashariki mwa nchi hiyo.
Hii ingekuwa katika mwaka ambao nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji.
Pia aliangazia umuhimu wa kuvutia uwekezaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
"DR Congo ina thamani ya $36tn [£27tn] katika madini... kazi yangu ni kutafuta wawekezaji ambao wanaelewa kwamba wanapaswa kutoa kwanza kabla ya kupokea, na kuwa na uaminifu wa hali ya juu kwa Rais Félix Antoine Tshisekedi."
Hata hivyo, baadhi wamehoji pasipoti mpya ya mwigizaji huyo, kwani katiba ya DR Congo inapiga marufuku uraia wa nchi mbili.