Mayele Awaonya Inonga, Onyango “Wakimpania Kumzuia Asifunge Watapigika Vibaya”




Mshabuliaji wa Yanga, Fiston Mayele akifanya yake.
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele, ni kama amewatahadharisha mabeki wa Simba kwa kusema wakiingia uwanjani kwa lengo la kumpania kumzuia asifunge, basi watapigika vibaya.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa Kariakoo Dabi utakaozikutanisha timu kongwe hapa nchini, Yanga dhidi ya Simba unaotarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni wa Ligi Kuu Bara ambapo hivi sasa Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 54, Simba inafuatia na pointi zake 41.

Safu ya ulinzi ya Simba ambayo imekuwa ikicheza mechi nyingi msimu huu inaongozwa na Hennock Inonga, Joash Onyango, Pascal Wawa, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.


 

Akizungumza na Spoti Xtra, Mayele alisema timu yao hivi sasa haimtegemei mchezaji mmoja katika kufunga, hivyo mabeki wa Simba wakiingia uwanjani kwa kumuangalia yeye pekee, basi watawapa wachezaji wengine nafasi ya kufunga.

Mayele alisema katika mchezo huo, kama Simba wakimpania yeye, basi Feisal Salum ‘Fei Toto’, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, Jesus Moloko na wengineo watakuwa na nafasi kubwa ya kufunga kutokana na uwezo walionao.

Aliongeza kuwa, kamwe hatabadili malengo yake aliyojiwekea ya kuwafunga Simba kama aliyoweka kuwafunga Azam FC na Namungo FC katika michezo iliyopita.


“Niliweka nia na malengo ya kuwafunga Azam na Namungo katika michezo ya ligi, lengo lilikuwa ni kuongeza idadi ya pointi zitakazotuwezesha kuchukua ubingwa.

“Ninashukuru kufunga michezo hiyo, hivyo hivi sasa nguvu na akili zangu zote ninazielekeza katika mchezo wa ligi dhidi ya Simba ambao ni mkubwa na wenye upinzani.

“Nikiwa katika malengo hayo ya kuwafunga Simba, kama ikishindikana basi watafunga wengine Fei Toto, Saido na Moloko ambao wapo bora.

“Ninafahamu kabisa katika mchezo huu mabeki wa Simba watakuja kwa lengo la kucheza kwa kunipania, lakini niwaambie kuwa waache wanikabe mimi halafu wawasahau wengine watakaokuja kuwafunga, kitu kikubwa tunachokihitaji Yanga ni kuchukua pointi tatu pekee,” alisema Mayele.


 
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Mayele hakufunga wakati timu hizo zikitoka suluhu, lakini kabla ya hapo, mshambuliaji huyo alifunga bao pekee kwenye ushindi wa 1-0 ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii msimu huu.

Mayele amefunga mabao 12 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ndiye kinara.

STORI; WILBERT MOLANDI

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad