Dar/Moshi. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameitaka Serikali kuwashughulikia watu wote waliolisababishia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha kama ilivyobainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mbowe alieleza hayo juzi katika Kata ya Sinza, wilayani Ubungo akiwa kwenye kampeni ya ‘Join the Chain’ yenye lengo la kuhamasisha wananchi kukichangia chama hicho kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kujiimarisha na kujijenga.
Hayo yanajiri siku chache baada ya CAG, Charles Kichere kuwasilisha ripoti yake bungeni ikibainisha upotevu na ubadhirifu wa fedha jumla ya Sh5.8 trilioni kwenye mashirika na taasisi za umma, Serikali za mitaa na Serikali Kuu.
Mbowe aliitaka Serikali kuwawajibisha watendaji wote waliolisababishia Taifa hasara hiyo wakati wananchi wakiendelea kukabiliana na ugumu wa maisha uliosababishwa na kupanda kwa bei za bidhaa.
“Niwape pole kwanza kwa sababu gharama za maisha zinazidi kuwa ngumu na kila kitu kinapanda, lakini serikalini bado kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha.
“Mmesikia taarifa ya CAG namna mabilioni yanavyoendelea kuvuja au kupotezwa kupitia mashirika ya umma na idara za Serikali.
“Hili jambo tunalikemea, ndio maana tunasema kuna ulazima wa kuwa na Bunge lenye vyama vingi litakaloisimamia Serikali kuliko Bunge la sasa. Tunaitaka Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za makusudi,” alisema Mbowe.
Alisema gharama za maisha zimezidi kuwa juu na baadhi ya bidhaa za vyakula zimepanda bei, hali inayosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kumudu. Kutokana na hali hiyo, Mbowe aliitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kupitia sera.
“Waangalie namna gani wanaweza kupunguza baadhi ya kodi na tozo, ili kuleta unafuu kwa Watanzania na kuwafanya waishi kwa furaha,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema tiba ya majeraha yaliyolikumba Taifa katika awamu tofauti za Serikali ni mabadiliko ya Katiba itakayozingatia haki na usawa kwa wananchi wote.
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja wakati kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kikikaribisha maoni au mapendekezo ndani ya siku 31 kuhusu maeneo tisa yaliyochambuliwa na kikosi hicho.
Alisema Chadema kitashirikiana na yeyote anayeona kuna ulazima wa kupatikana kwa Katiba mpya sasa na si baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 kama ambavyo kikosi kazi kinachoongozwa Profesa Rwekaza Mukandala kimependekeza.
“Tutafanya mazungumzo na wote wanaohusika kuitafuta haki hiyo na si haki ya Chadema, bali haki ya Watanzania wote, ili tujenge Taifa ambalo katiba yetu inatibu majeraha na inanyoosha mstari wa maendeleo,” alisema.
Mbowe alisisitiza Katiba mpya itakomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na baadhi ya viongozi waliolewa madaraka.
“Tunahitaji katiba ambayo itajenga taasisi imara za Bunge na Mahakama katika nchi yetu, itakayohakikisha haki kwa watu wote na si wanasiasa pekee,” alisema.
CAG na vyama vya siasa
Katika ripoti hiyo, CAG pia amevinyooshea kidole vyama vya siasa nchini kwa upungufu mbalimbali, ikiwamo kukiuka sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019.
Maeneo mengi ambayo vyama hivyo vimeguswa na ripoti hiyo kwa mwaka 2020/2021 inayoishia Juni 30, 2021 yanaangukia katika masuala ya fedha na vyama kuchelewa kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya ukaguzi.
Taarifa imetaja maeneo mengine ni baadhi ya vyama kufanya malipo bila viambatanisho, kutowasilisha tamko la mali, CCM na migogoro ya ardhi, vituo 30 vya redio kurusha matangazo ya CCM bila mikataba na kampuni za CCM kutotoa gawio.
Mbali na maeneo hayo, taarifa hiyo ya CAG imebainisha maeneo yenye upungufu kuwa ni Chadema kushindwa kurejesha deni la mkopo, CUF kutotoa taarifa ya umiliki magari saba na malipo kufanywa bila kufuata taratibu.
CCK, NLD, UDP kikaangoni
CAG alisema ingawa idadi ya vyama vilivyochelewa kuwasilisha taarifa zao za fedha imepungua kutoka vitano hadi vitatu, vyama vya CCK na NLD bado havijawasilisha taarifa za kifedha hadi Septemba 30, 2021.
“Ni maoni yangu mapendekezo yangu ya mwaka uliopita (2019/2020) hayakutekelezwa na kwa sababu hiyo, muda wa ukaguzi wangu haukutekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa kalenda ya ukaguzi,” ilieleza taarifa hiyo.
CAG amependekeza Msajili wa Vyama vya Siasa ahakikishe vyama vinawasilisha taarifa za fedha ofisi ya CAG kwa wakati kabla ya Septemba 30 ya kila mwaka na pia kuchukua hatua stahiki dhidi ya vyama vya UDP, CCK na NLD.
Kwa mujibu wa CAG, vyama vimeshindwa kuzingatia Kifungu cha 18A (2) (a) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 (iliyorejewa mwaka 2019).
CCM na mashauri ya Sh3.6 bil
Kulingana na taarifa ya CAG, CCM ina mashauri 108 yaliyofunguliwa na wadai mbalimbali yanayoendelea katika mahakama tofauti yenye thamani ya Sh3.63 bilioni.
Kati ya kesi zilizofunguliwa, 86 zinahusu migogoro ya ardhi, kesi 12 zinahusu kazi na 10 zinahusu madai zenye thamani ya jumla ya Sh3.63 bilioni.
“Kikubwa zaidi nilibaini CCM kina kiwango kikubwa cha kesi za ardhi ikilinganishwa na kesi nyingine zilizo katika ngazi tofauti za mahakama, zenye mamlaka ya kuamua migogoro ya ardhi kama ilivyobainishwa na sheria,” alisema CAG.
Katika ukaguzi wake, CAG alisema alibaini kasi ya ongezeko la kesi za ardhi inachangiwa na kuchelewa kutatua migogoro ya ardhi kutokana na kukosekana kwa mfumo mzuri wa utatuzi wa migogoro ya ardhi ndani ya CCM.
Menejimenti ya CCM ilisema walikuwa na kesi na mashauri 112 yenye thamani ya Sh4.14 bilioni mwaka jana ikilinganishwa na kesi 108 zenye thamani ya Sh3.63 bilioni mwaka huu, hivyo kumekuwa na uboreshaji.
“Ninapendekeza CCM ianzishe mfumo wa utatuzi wa migogoro na kuboresha kitengo chake cha sheria, ili kesi zake ziweze kusuluhishwa kwa njia za maelewano,” alishauri CAG.
Malipo ya Sh146.3 milioni
Katika uhakiki uliofanyika katika vyama 19 vya siasa, CAG alibaini vyama vitano vililipa Sh146.39 milioni kwa ajili ya malipo mbalimbali, lakini hakuna kumbukumbu zinazotunzwa.
Kutokana na hilo, CAG alisema hakuweza kuthibitisha uhalali wa matumizi yaliyofanywa na akataja vyama hivyo kuwa ni ADC (Sh5.7 milioni), NRA (Sh16.7 milioni), AAFP (Sh31 milioni), Chadema (Sh37 milioni) na CUF Sh55.7 milioni.
Pamoja na vyama kufanya uboreshaji, bado CAG amependekeza maofisa masuuli wa vyama vya siasa kuhakikisha udhibiti wa ndani unasimamiwa ipasavyo kwa kila malipo yanayofanyika yawe na nyaraka husika.
CUF nayo yaguswa
Katika ukaguzi huo ilibainika kuna kesi iliyofunguliwa dhidi ya CUF kuhusu umiliki wa magari haijaripotiwa katika taarifa zake za fedha Sh873.3 milioni.
Kwa mujibu wa CAG, CUF huandaa taarifa zake za fedha kwa kufuata mwongozo wa viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS).
CUF kinatakiwa kuripoti madai yake yaliyoko mahakamani yanayosubiri uamuzi na kuna uwezekano wa CUF kutangazwa kama mshtakiwa na kupaswa kumlipa mlalamikaji au mdai.
Hata hivyo, kupitia majalada ya kisheria ya CUF, CAG alibaini mojawapo ya kesi zilizofunguliwa Mahakama Kuu Septemba 2019 dhidi ya CUF.
Katika uchunguzi zaidi, aligundua CUF ilipewa hati ya madai na mojawapo ya kampuni ya kisheria kusalimisha magari saba yaliyodaiwa kuchukuliwa na CUF kutoka kwa mmojawapo wa wanachama wake.
Pamoja na kusalimisha magari hayo, CUF pia kilitakiwa kulipa fidia ya Sh873.3 milioni ili kumfidia mdai kutokana na usumbufu na hasara aliyoipata, lakini wakati wa ukaguzi Januari 2022, CUF kilikuwa bado hakijaweka wazi suala hilo katika taarifa zake za fedha.
Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Juma Isihaka na Bakari Kiango (Dar).