Dodoma. Wakati wabunge wakieleza kukerwa na ucheleweshaji wa mafao ya watumishi wa umma, Mbunge wa Nyasa (CCM), Stella Manyanya amewaonya wapambe wa viongozi, maarufu kama chawa (wapika majungu) wanaowasema vibaya viongozi waliopita na waliopo, akisema hali hiyo haileti afya kwa Taifa.
Manyanya alitoa kauli hiyo bungeni jana, wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2022/23, huku akiwataka kuacha mambo hayo kwa sababu Taifa lisingefika hapa lilipo bila viongozi waliopita na haliwezi kuendelea bila viongozi.
“Sasa badala ya kushikamana, tunapigana na tena wanaopigana ni chawa, kuna chawa wa viongozi wa zamani na chawa wa viongozi wa sasa.
“Ukiangalia kwanza neno lenyewe chawa linanitia kizunguzungu, kwanza akikuingia anaweza akanyonya zaidi akakuharibia hata maisha. Kwa hiyo mimi nasema hawa chawa wasaidie Taifa liende mbele,” alisema Manyanya, aliyewahi kuwa naibu waziri katika wizara mbalimbali na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Alisema anataka kuona watu wanaosifia kuhusu mazuri yaliyofanywa na viongozi waliopita na wale wa sasa.
ADVERTISEMENT
Watumishi 8,000 kupanda vyeo
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Waziri Jenista Mhagama alisema katika mwaka wa fedha 2022/23 watumishi 8,080 wametengewa nafasi za kubadilishwa vyeo ambao wataigharimu Serikali Sh2.21 bilioni katika mwaka huo wa fedha.
Alisema utekelezaji wa kazi ya kuwapandisha vyeo katika mwaka huo utakuwa kwa watumishi 120,210 ambao watalipwa Sh42.39 bilioni.
Pia alisema wizara hiyo itasimamia ajira za watumishi wapya 30,000 katika kada mbalimbali ambao wataigharimu Serikali Sh120.77 bilioni.
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeliomba Bunge kuwaidhinishia Sh851.08 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/23.
Wabunge wacharuka
Wabunge walicharukia Serikali kuhusu ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu na upungufu wa watumishi wa umma, huku wakipendekeza kufanyika kwa ukaguzi wa kitaifa wa nguvu kazi hiyo.
Akichangia, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya alisema bado wastaafu wanacheleweshewa mafao yao kwa madai kuwa majalada yao hayajafanyiwa kazi.
Alisema hadi hata kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inaonyesha kuwa kuna majalada 571 hayajafanyiwa kazi.
Alisema wastaafu ambao wamekaa miaka mitatu bila kulipwa mafao yao ni watumishi 391, waliokaa miaka mitano bila kulipwa 59, waliokaa miaka 10 wapo 54 na waliokaa miaka 20 ni 17.
Wastaafu wengine waliokaa miaka 15 wapo 25, miaka 25 wapo 18 na miaka 28 wapo saba.
“Wastaafu waliotumikia nchi hii kwa jasho na damu bado hawajalipwa mafao yao, huku watumishi hatuwapandishi madaraja na tukiwapandisha mlundikano wa madai yao tukiwaajiri malimbikizo ni lukuki,” alisema.
Alitaka Serikali kuwatendea haki watumishi wanaolitumikia Taifa kwa jasho na damu na kwamba wamekaa miaka mitano bila kupandishiwa mishahara, lakini wamekuwa wakifanya kazi bila kulalamika.
Akizungumzia upungufu wa watumishi wa umma, Profesa Kitila Mkumbo (Ubungo-CCM) alisema sekta ya elimu kwa mujibu wa taarifa za Serikali, mahitaji ya walimu wa msingi na sekondari ni 433,992, lakini waliopo ni 258, 291 huku upungufu ikiwa walimu 175,701 ambao ni sawa na asilimia 40. Kwa upande wa sekta ya afya, alisema watumishi wanaohitajika ni 208,232 lakini waliopo ni 98,987 ambapo pungufu ni watumishi 109,295 sawa na asilimia 52.5.
Alisema hali ni mbaya katika zahanati na vituo vya afya ambako asilimia 70 ya Watanzania ndiko wanakopata matibabu.
Alisema katika maeneo hayo kuna upungufu wa asilimia 63.1 wakati kwenye maji watumishi wanaohitajika ni 10,276 na waliopo ni watumishi 9,207.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, mahitaji ni watumishi 20,000 waliopo ni 6,600 na upungufu ni 13,400 sawa na asilimia 67.
Profesa Mkumbo alisema kwa sekta hizo mahitaji ya watumishi wa umma ni 1,023,889 na watumishi waliopo ni 679,955 hivyo kufanya kuwepo na upungufu wa watumishi 558,134, sawa na asilimia 45.
Alisema Serikali imetoa taarifa kuwa itaenda kuajiri watumishi 30,000 katika mwaka huu wa fedha, jambo ambalo linaonyesha wataenda kutatua tatizo kwa asilimia 4.4.
Profesa Kitila alishauri kufanyika ukaguzi wa kitaifa wa watumishi wa umma, ili kupata mahitaji halisi ya watumishi wa umma nchini.
Alisema alipokuwa Wizara ya Maji kama katibu mkuu aligundua kuna kazi moja inayofanywa na wafanyakazi wawili.
Alitaka utekelezaji wa ugatuaji wa madaraka kikamilifu na kuweka mazingira mazuri, ili watu waanzishe shule na vituo vya afya vya kutosha.
Janejelly Ntate (Viti Maalum-CCM) alisema utaratibu wa kuajiri sasa unafanya watu waliomaliza vyuo miaka ya karibuni kupata ajira na kuwaacha wale waliomaliza miaka iliyotanguliwa.
“Kama walioomba ni 20,000 na wakapata kazi 1,000 ukitangaza nafasi nyingine chukua kwenye database. Hii itasaidia kuajiri kutokana na umalizaji wa vyuo,” alisema. Aidha, aliomba teuzi za mamlaka zinapokoma watumishi wapangiwe maeneo ya kazi mapema, ili kuepuka hasara na maumivu kwa watumishi hao.
“Teuzi hizi zinapokoma wanachelewa kupangiwa kazi na Serikali inapata hasara, lakini kwa mtumishi kupata msongo, ulevi na kufa kifo amchacho hakikupangwa na Mungu. Nawaomba wapangiwe mapema,” alishauri.
Kamati yaja na mapendekezo
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chaurembo alishauri Serikali kuendelea kuimarisha misingi ya utawala bora, mishahara na maslahi ya watumishi wa umma.
Pia alishauri Serikali kuboresha miundombinu, maendeleo ya watumishi na mifumo ya utendaji kazi katika utumishi wa umma.
“Watumishi waendelee kuhimizwa kuwa wazalendo kwa nchi yetu na kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, weledi na maarifa kama msingi imara wa maendeleo,” alisema.
Aidha, kamati hiyo ilishauri Serikali iendelee kutoa ajira zaidi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi.