By Sharon Sauwa
Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu amesema wanaume wengi hawana uwezo wa kumudu kugharamia mapenzi, hali inayowafanya wakimbilie kwa watoto wasio na hatia na kuwafanyia ukatili wa kingono.
Jesca amesema hayo leo Aprili 14, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) 2022/2023, akisema zipo sababu zinazosababisha wanaume kuwabaka watoto wadogo ikiwemo ukata na ushirikina.
“Mapenzi ni product (bidhaa) kama product nyingine, vijana hawana nguvu ya kununua wanakwenda kwa watoto wadogo na kuwaonea. Kwa nini wamepunguza nguvu ya kununua mapenzi ni kwasababu ya ukatili wa kiuchumi ikiwemo na sisi hapa tunachangia,” amesema.
Amesema kama kuna wizara ambayo haiwezi kutoa kipaumbele kwa watanzania katika miradi inayotekelezwa na Serikali hao ndio wanaosababisha matatizo hayo ya ukata na ukatili wa kijinsia.
Bila kutaja aliyesema, Jesca alisema mtu anaposema nguzo zote zinunuliwe nje ya nchi, vijana waliopanda miti katika mikoa mbalimbali watapata wapi fedha za kununua mapenzi watakapokuwa na hitaji la mapenzi.
“Sasa hivi hakuna mwanamke atakupenda sura kwasababu hakuna mwanaume mwenye sura nzuri. Unampendaje mwanaume sura mwanaume. Mwanaume anapendwa kitu alichonacho anapendwa fedha,” amesema.
Amesema wanaume rijali wataenda wapi na anahamu ya kufanya mapenzi.
“Mnakwenda kuwabana wamachinga badala ya kuwajengewa mazingira mazuri ya kufanya kazi wawe na uwezo wa kununua penzi,” amesema.
Amesema kama sababu ya ushirikiana hiyo inashughulikiwa kiroho kwa kutumia nguvu za Mungu.
Jesca akawataka wabunge wanaoamini kufuatana naye katika dua fupi aliyoitoa bungeni wakati akichangia.
“Mungu tusaidie, hatutawaasi kama alivyosema mheshimiwa (mbunge mmoja alitaka waasiwe wanaohusika na ukatili huo) lakini tuachilie nguvu za Mungu kuanzia hapa zikawashughulikie wote.
“Katika kile kiungo wanachotumia kulawiti watoto wetu kipigwe nguvu kisifganye kazi na zile mashine mbili zinazozalisha nguvu zipotee kabisa na daktari utakapoona dalili hizo anitafute. Arudi katika hali ya kawaida tumfanyie ushauri nasaha ili watoto wetu wawe salama,” amesema.
Awali Jesca amesema takwimu alizozitoa waziri (bila kumtaja) zinaonyesha kuwa asilimia 33 wanaofanyiwa ukatili ni watoto na asilimia 67 ni wanawake.
Hata hivyo, amesema upo ukatili pia dhidi ya wanaume na tafiti zinaonyesha kuwa kiwango cha wanaume kupigwa kimeongezeka hadi asilimia 71.7 wakati wanawake wamepigwa kwa asilimia 73.5.
“Na kwakiwango hichio wanaume wanashuka kwa kukipa na wanawake wanapanda kwa kasi kubwa,” amesema.
Amesema kwa hali inavyoendelea inaonekana kuwa athari zinawaangukia watoto kwasababu wanavyoendelea ustamilivu unakuwa haupo na hivyo kuweka mazingira hatarishi kwa watoto.
“Kati ya asilimia 33 ya watoto wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wa kiume ni asilimia 11.5 na asilimia 22 kwa wa kike. Na hawa wanaume ina maana ukatili waliofanyiwa wameingiliwa kinyume cha maumbile,”amesema.
Amesema wasichangae baada ya miaka 10 mtoto wa kiume anafika nyumbani na mkwe wa kiume mwenzie.
“Tukisema Astaghfirulah Mungu atakuwa hajakuepushia. Kati ya watoto waliofanyiwa ukatili asilimia tatu ndio waliopata ushauri nasaha na kutibiwa na 13 kwa wanawake walipata ushauri nasahi na kutibiwa,”amesema.
Mwananchi