Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, David Kihenzile ameleza namna safari ya mwisho kabla ya kifo cha mbunge mwenzao Iren Ndyamkama kwamba alizuiwa kusafiri kwa ndege kutokana na hali yake.
Kihenzile amesema walikuwa na safari ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya ukaguzi wa viwanda na walipofika uwanja wa ndege wa Dodoma mwenzao alizuiwa kupanda ndege kutokana na hali yake.
Kihenzile ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 27, 2022 wakati akitoa salamu kwa niaba ya kamati ya Viwanda ambayo marehemu Iren alikuwa mjumbe.
“Kutokana na hali yake, pale Airport walimzuia kusafiri kwa ndege lakini akasema lazima aende Dar es Salaam ndipo aliamua kuanza safari kwa kutumia gari lakini ghafla tukapata taarifa za msiba wake,” amesema Kihenzila bila kutaja hali yake ilikuwaje.
Amesema baada ya kuona hatosafiri na wajumbe wenzake, alianza kuwafuata mmoja mmoja na kusalimiana naye kisha akaamua kuanza safari akiwaambia kuwa wangekutana huko ili wafanye kazi ya wananchi.
Hata hivyo mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudensia Kabaka amesema kuwa Iren alikuwa ni mjamzito na kwamba kuna mambo mengi aliyokuwa ameyapanga kuyafanya baada ya kujifungua.
Kabaka amesema kutokana na hali ya ujauzito aliyokuwa nayo, alisimamisha baadhi ya mambo ikiwemo ujenzi wa nyumba ya Katibu wa umoja huo mkoa wa Rukwa ambayo alikuwa ameahidi kuijenga lakini alikwenda kumwambia kuwa ataifanya kazi hiyo alishajifungua.
Ndyamkama alifariki Aprili 24, 2022 katika hospitali ya Tumbi Kibaha alikokwenda kupatiwa matibabu baada ya kuugua akiwa safari kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam na ameacha mume na watoto watatu