MBUNGE wa chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luhaga Mpina amesema, atatumia mkutano huu wa Bunge la Bajeti unaoendelea kuelezea mambo makubwa ya nchi ikiwemo ucheleweshaji wa mradi wa Bwawa wa kufua umeme la Julius Nyerere.
Mpina aliyewahi kuwa waziri wa mifugo na uvuvi amesema, hatoogopa mtu wala kikundi cha watu kuzungumzia mambo yenye maslahi mapana ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari amesema, kumekuwa na tabia ya baadhi ya mawaziri kutokujibu kwa ufasaha hoja zinazoibuliwa na wabunge pamoja na wananchi jambo ambalo halipaswi kuachwa likaendelea.
“Rais (Samia Suluhu Hassan) amebaini baadhi ya mawaziri matapeli na waongo, wanapeleka maneno ua uongo, unaulizwa swali la mbunge kuchelewa kwa mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere au mfumko wa bei unakwemwa kusema unaishambulia serikali. Mimi nauliza maswali ya wananchi si ya nyumbani kwangu,” amesema Mpina na kuongeza:
“Bunge la Bajeti limeanza, nimejiandaa vizuri, nimejipanga na nitaweka wazi baadhi ya hoja ngumu za wananchi ikiwemo kuchelewa kwa Bwawa la umeme, kukatikakatika kwa umeme, kupanda kwa bei za bidhaa, kuchafuka kwa mto mara. Tutakwenda kuyasema yote bila kumwogopa mtu, bila vitisho kutoka kokote.”
Aidha, amempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ya kulinda Katiba, sheria na taratibu za nchi kwenye uongozi wake na kuahidi kwamba atamsaidia kwa kueleza ukweli masuala mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi na Taifa.
Mwanahalisionline