Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde amemshukia Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na watu wanaomsema vibaya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli na kumsema vizuri Rais Samia Suluhu Hassan ni wanafiki kwa sababu watamgeuka Rais Samia pindi atakapoondoka madarakani.
Kauli ya Lusinde imekuja baada ya hivi karibuni Zitto alikaririwa kwenye mitandao ya kijamii akiwakosoa wanaomsifia Hayati Rais Magufuli.
Lusinde ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 22, 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi ya Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2022/2023, ambapo amesema licha ya ushirikiano uliopo kati ya vyama vya CCM na ACT Wazalendo visiwani Zanzibar, ameshangazwa na Zitto kumnanga Hayati Magufuli kana kwamba Zitto hashiriki katika Serikali ya Zanzibar.
“Nataka niseme Marehemu Magufuli aheshimiwe, kufiwa ni suala kubwa haiwezekani kulizungumza kwenye utawala bora suala la Magufuli kusemwa vibaya na mimi sitaacha.
“Zitto anatutaka tunaompenda Magufuli tukazikwe naye. Zitto amewahi kufiwa na mama yake mimi sitaki kuingia huko mama wa Zitto ni mama yangu mimi ametanguliwa. Mimi nimewahi kufiwa na baba yangu lakini ACT Wazalendo wamewahi kufiwa na Maalim Seif wanataka tumseme vibaya sisi hatuwezi,”amesema.
Amesema wengi wa wabunge ni waislamu wamefungwa na dini inakaata kuwasema vibaya marehemu na Zitto anajua hilo.
Amesema Zitto amewakosea sana Watanzania, Mke na familia ya Magufuli anatakiwa kuwaomba radhi kwa kitendo chake cha kumnanga Magufuli.
Amesema wasifikiri kumsema vibaya Magufuli kutawasaidia kwasababu ameshafariki dunia na kwamba kama mtu alikuwa na tatizo naye amalize watakuja kukutana naye kwa Mungu.
“Mtu akishatangulia kitabu chake kinafungwa tunamuachia mwenyezi Mungu kuja kutoa hukumu inakuaje viongozi wakiwepo hamsemi wakiondoka mnasema huo ni uoga uliopitiliza,”amesema.
Lusinde amesema mtu mmoja alisema kwa vitendo kuwa hawezi kufanya kazi na Magufuli naye alikuwa ni Nyalandu (Lazaro Nyalandu aliyewahi kuwa Mbunge wa Singida Kaskazini na Waziri wa Maliasili na Utalii).
“Lakini wote tuliobaki hapa ni watu wa Magufuli, na tulifanya naye kazi na tulikuwa tunamsifu na hivyo ndivyo tunatakiwa kumsifu na mheshimiwa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan). Ndio kazi tunayoifanya hapa hatufanyi unafiki.
Nataka nikwambie hawa watu wanaomsema vibaya Magufuli na kumsifu Rais Samia ni wanafiki wakubwa. Samia akiondoka watamsema vibaya hivyo hivyo, ni bora mimi Lusinde niko wazi. Na siwezi kuacha haiwezekani.”amesema.Amesema kwamba ili nchi iendelee utawala bora watu wote ni lazima kushirikiana nao na kwamba hao waliofariki dunia ni watu wazito.
Amehoji kauli ya wanaompenda Magufuli wakazikwe naye maana yake ni nini na kumtaka Zitto kuomba radhi na asirudie tena kusema maneno hayo ya kipuuzi.