Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema ajira mpya 32,604 zinazotarajiwa kutangazwa kabla ya kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, zitaigharimu Serikali Sh. bilioni 315.570 kwa mwaka. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Mhagama ametoa kauli hiyo leo tarehe 12 Aprili, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utoaji wa vibali vya ajira kwa watumishi wa umma nchini.
Amesema kati ya ajira hizo 32,604, sekta zilizopewa kipaumbele ni elimu iliyopewa nafasi12,035, afya 10,285 na sekta zingine nafasi 2,392.
Amesema katika nafasi 12,035 za sekta ya ellimu, nafasi 9,800 ni kwa wa walimu wa shule za msingi na sekondari, ambapo mchakato wake utasimamiwa na TAMISEMI ilihali nafasi 2,235 ni kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu, vyuo vya elimu ya juu na wakufunzi wa vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo mchakato utasimamiwa na taasisi husika kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Kwa upande wa sekta ya afya, Mhagama amesema imekasimiwa nafasi za ajira 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo mchakato utasimamiwa na TAMISEMI.
Amesema nafasi 1,650 kwa ajili ya watumishi wa kada za afya katika Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo mchakato wake utasimamiwa na Wizara ya Afya.
Pia amezitaja nafasi 1,023 kwa ajili ya vyuo vya afya, hospitali nyingine za kimkakati na zile za Mashirika ya Dini (District Designated Hospitals-DDHs) na hiari (Voluntary Agency-VAHs) zenye mkataba na Serikali.
“Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Wizara ya Afya kwa Vyuo vya Afya na Hospitali nyingine za kimkakati na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kwa Hospitali za DDHs na VAHs,”amesema.
Mhagama pia amefafanua nafasi 2,392 zinazotarajiwa kujazwa kwenye sekta zingine za kipaumbele kuwa katika kada za Kilimo nafasi za ajira ni 814, kada za mifugo nafasi 700, kada za uvuvi nafasi 204, kada za maji nafasi 261 na kada za sheria nafasi 513.
Amesema chakato wa ajira hizo utasimamiwa na wizara husika pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Waziri amefafanunua kuwa zipo nafasi 7,792 kwa ajili ya watumishi wa kada nyingine kwenye wizara, idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma.
Mchakato wake utasimamiwa na wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
92,619 KUPANDISHWA MADARAJA
Pia Mhagama amesema katika kipindi hicho Serikali itawapandisha vyeo/madaraja watumishi 92,619 ambapo itatumia jumla ya Sh. bilioni 276. 938 kwa mwaka kuwalipa mishahara.
Amesema katika kuwabadilisha vyeo/kada watumishi 6,026 waliotengewa Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuanzia 01 Mei, 2022, gharama zake ni Sh. bilioni 9.893 kwa mwaka.
Pamoja na mambo mengine amesema kwa sasa mahitaji ya watumishi kwa taasisi za Umma yapo kati ya asilimia 52 hadi 90.
Amesema ajira hizo ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kuhakikisha utekelezaji wa wake unakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 haujaisha.
Aidha, Waziri aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa ajira hizi ili kuweza kubaini na hatimaye kuzuia mianya yote ya rushwa na upendeleo.