Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameilaumu jumuiya ya kimataifa kwa kuelekeza nadhari zaidi juu ya vita vya Ukraine, na kuhoji kuwa mizozo kwingineko, ikiwemo katika taifa lake la nyumbani Ethiopia, haipewi uzingativu sawa, yumkini kwa sababu wale wanaoteseka siyo weupe.
"Sijui kama ulimwengu unayazingatia kwa usawa maisha ya watu weusi na weupe. Nilisema wiki iliyopita, nadhari yote kwa Ukraine ni muhimu sana pasina shaka, kwa sababu inaathiri dunia nzima.
Lakini sehemu yake ndogo tu haitolewi kwa Tigray, Yemen, Afghanistan, Syria na kwingine. Sehemu tu," alisema Tedros, wakati akizungumza katika mkutano wa vidio kutokea Geneva jana Jumatano.
Mwezi uliyopita Tedros alisema hakuna popote duniani, ambako afya ya mamilioni ya watu inakabiliwa na kitisho kikubwa kuliko mkoa wa Ethiopia wa Tigray, akidai kuwa malori 20 tu ya msaada ndiyo yemeruhusiwa kuingia mkoani humo tangu kutangazwa kwa mapatano wiki tatu zilizopita, badala ya takribani malori 2,000.