MABOSI wa Yanga, wanabadilisha anga wakisaka vifaa vipya vya kigeni kwa malengo ya msimu ujao, lakini ndani ya timu yao kumeibuka mshtuko mmoja mkubwa, baada ya Bilionea Mohamed Dewji ‘MO’, kutangaza vita moja kubwa akitaka kumchukua beki na nahodha wao Bakari Mwamnyeto.
Taarifa zilizothibitishwa na Meneja wa Mwamnyeto ni kwamba, Simba inatafuta beki wa maana wa kati na imeamua kuanza na hapa hapa ndani, wakitua Yanga wakitaka kwa gharama yoyote saini ya beki huyo wa shoka mwenye mwili jumba.
Ofa ya Simba, imetoka kwa MO, akivutiwa na huduma ya Mwamnyeto katika miaka miwili ambayo amedumu Yanga, ili aje achukue nafasi ya Pascal Wawa, ambaye mwisho wa msimu huu kuna uwezekano mkubwa akapewa mkono wa kwaheri.
Meneja wa Mwamnyeto, Kassa Mussa ambaye anaishi Italia, amelitithibitishia Mwanaspoti, akisema Simba imekuwa ikimsumbua ikidai inataka kuweka rekodi ya maumivu kwa watani wao.
“Simba wanasumbua sana nisiseme uongo, wamekuwa wakiibuka na ofa kubwa kubwa na dhamira yao wamekuwa wakiniambia wanataka kupeleka kilio kule Yanga na ofa yao ni kubwa hasa ambayo nayo tumeamua kuichukua na kuendelea kuifanyia kazi,” alisema Kassa ambaye ni nyota wa zamani wa Coastal Union.
“Ukiacha Simba, Bakar ana ofa nyingi sana, kuna ofa tatu au nne hivi, kuna klabu ya Ugiriki, Malta na nyingine moja bado tunazungumza nazo, lakini kwa hapo Tanzania kuna Yanga inayohitaji kumbakisha, Simba yenye kasi na Azam FC.”
Hata hivyo, Kasa alisema Yanga wenyewe hawako nyuma na kwa kuwa, bado mkataba unawaruhusu, wamekuwa wakipambana kumbakiza nahodha wao ambapo mazungumzo hayo yanafanyika chini ya Injinia Hersi Said.
“Mazungumzo yetu yanakwenda vizuri sana, Unajua Yanga ndio klabu ambayo mchezaji bado yupo na ni vyema ukawapa heshima yao hadi mkataba utakapoisha Agosti mwaka huu,” alisema Kassa na kuongeza;
“Nimekuwa sina shida nao Yanga nisiseme uongo, kuanzia walivyompokea Bakari, wakampa unahodha na kumpa muda wa kutosha nahodha wao, kifupi Yanga hatuna shida nao imekuwa ni miaka miwili yenye maendeleo mazuri kwa mchezaji wangu.
“Ilikuwa nije mapema lakini bahati mbaya nilipata ajali, Yanga na hata hao Simba walikuwa wananisubiri mimi ili tuje kufanya maamuzi, nimepanga nikishakuwa sawa mpaka mwishoi wa mwezi huu nitaanzia kwanza Ugiriki kisha nije huko.”