MASTAA muhimu wa Simba, Bernard Morrison na wenzie watano akiwamo Aishi Manula na Erasto Nyoni wamefutiwa kadi zao kikanuni hivyo mechi ijayo ya CAF dhidi ya Orlando Pirates ni ruksa.
Wengine ni Henock Inonga, John Bocco, Meddie Kagere, Pape Sakho, Peter Banda, Serge Wawa na Taddeo Lwanga.
Simba itawakosa Joash Onyango na Sadio Kanoute tu katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao utachezwa Jumapili saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kanuni za mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika zimewapa nafuu wachezaji hao ambao kila mmoja ameonyeshwa kadi moja ya njano katika hatua ya makundi ambapo zinafafanua kuwa mchezaji ambaye amepata idadi ya kadi ambazo hazimfanyi akose mechi inayofuata, atafutiwa kadi zake iwapo timu itaingia katika hatua inayofuata.
Kanoute na Onyango wao wamejikuta wakikosa mechi ya kwanza itakayochezwa hapa Tanzania kwa vile wao kila mmoja ameonyeshwa kadi za njano mara tatu jambo ambalo kwa mujibu wa kanuni, linawafanya wakose mechi inayofuata ingawa wangeweza kupona na kadi zao kufutwa iwapo wangepata chini ya idadi hiyo.
“Mchezaji aliyepata kadi tatu za njano atakosa moja kwa moja mchezo unaofuata wa mashindano ya klabu ya Caf. Kusimamishwa huko moja kwa moja kunapaswa kutolewe taarifa na sekretarieti kwenda kwa vyama husika.”
Mwishoni mwa hatua ya makundi, kadi za njano ambazo hazipelekei mchezaji kusimamishwa zitafutwa,” inafafanua kanuni ya saba ya mashindano hayo.
Kitendo cha wachezaji hao kufutiwa kadi hapana shaka kitakuwa na faida kwa Simba hasa katika mchezo wa marudiano ugenini ingawa atakosekana mchezaji mmoja tu, Bernard Morrison ambaye yeye hatosafiri kwenda Afrika Kusini kutokana na sababu za kisheria. Meneja wa Simba, Patrick Rweyemanu aliliambia Mwanaspoti kuwa kufutwa kwa kadi kwa wachezaji wao hakuleti tofauti yoyote.