MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema na mkewe Doreen Kimbi, wameibua shangwe walipoingia katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kumlazimu Rais Samia Suluhu Hassan kukatisha hotuba yake kwa muda kupisha shangwe hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Mrema na Mkewe waliofunga ndoa hivi karibuni katika Parokia ya Uwomboni, Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro, waliibua shangwe hizo wakati wanaingia kwenye mkutano huo unaoendelea jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM Jakaya Kikwete.
Mrema na mkewe waliingia ukumbini hapo wakati Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan, anafungua mkutano huo, ambapo alilazimika kukatisha hotuba yake kutokana na kelele za shangwe.
Kufuatia kelele hizo, Samia ambaye ni Rais wa Tanzania, alilazimika kuwapa salamu ya CCM wajumbe, kisha akasema “bwana harusi na bibi harusi oyee! Tuendelee.”
Baada ya Rais Samia kumaliza kutoa hotuba yake ya ufunguzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka, alimtambulisha Mrema na Doreen akisema “aliyeingia muda mfupi ni ndugu Augustino Mrema akiwa na Mama Mrema.”
Awali katika hotuba yake, Samia aliwaomba wajumbe wa mkutano huo wapitishe kwa kauli moja ajenda zote, ambazo ni kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya CCM ya 1977, toleo la 2020.
Pamoja na kumpitisha Abdulrahman Kinana, kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, baada ya kupendekezwa jana na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kugombea nafasi hiyo kufuatia hatua ya aliyekuwa anaishikilia Mzee Phillip Mnagula, kujiuzulu.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan
“Bila shaka mtakubaliana na mimi ajenda hizi ni za muhimu sana, sio tu kwa uhai na maendeleo ya chama, bali kwa maendeleo ya Taifa. Mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake, vifungu vinavyofanyiwa marekebisho vinahusika moja kwa moja,”
“Na vitatumika katika kujaza nafasi za wajumbe katika chaguzi mbalimbali za CCM. Kwa mnasaba huo kazi tunazofanya leo ni sehemu ya maandalizi ya chaguzi za chama na jumuioya zake,” amesema Samia.
Aidha, Samia aliwaomba wajumbe wa mkutano huo ambao hawajapata chanjo ya Ugonjwa wa Uviko-19, kupata chanjo hiyo katika mabanda yaliyokuwepo nje ya ukumbi huo.
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, amesema mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 1,875 kati ya 1,889 sawana asilimia 99.2 ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.