DOREEN Reguna almaarufu Queen Magali; ni mkongwe kwenye tasnia ya Bongo Muvi ambapo aliwahi kujizolea umaarufu na Kundi la Mishemishe ambaye hivi karibuni alifanyiwa unyama na vibaka wanaopora kwa kutumia pikipiki wanaojulikana kwa jina la vishandu.
Queen Magali alikumbwa na mkasa huo kwenye Barabara Saba jijini Tanga ambapo anaishi kwa sasa. Katika tukio hilo, inadaiwa kuwa mwigizaji huyo, akiwa kwenye mishemishe zake ndipo wakatokea vijana wawili mbele yake waliokuwa wamepakizana kwenye bodaboda, lakini yeye hakuwajali akijua wako kwenye mambo yao.
Inaelezwa kuwa, vijana hao walimpita, lakini kumbe walikuwa wakimpigia hesabu ambapo baada ya muda waligeuza bodaboda hiyo na kuanza kumfuata kwa nyuma.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, Queen Magali anasema ghafla katika hali ya kushtukiza alijikuta akiporwa mkoba, lakini alijitahidi kuung’ang’ania ndipo vishandu hao walianza kumburuza na bodaboda barabarani huku akiwa ameendelea kuung’ang’ania mkoba huo uliokuwa na simu na mazagazaga mengine.
Hata hivyo, Quuen Magali anasema wakati purukushani hiyo ikiendelea, kwa kuwa ilikuwa ni muda wa jioni kulikuwa na watu wengi ambao waliingilia kati na kumsaidia kupiga mayowe ya wezi ndipo waliuachia mkoba huo na kufanikiwa kukimbia.
Baada ya kuponyoka kwenye tukio hilo, Queen Magali anasema alijikuta amebaki ma michubuko iliyotokana na kuburuzwa barabarani na kujigonga sehemu mbalimbali za mwili wake wakati akiburuzwa. Baada ya tukio Hilo alikwenda kupata matibabu kwenye Hospitali ya Bombo kisha kwenda kuripoti Polisi.
Stori; Richard Bukos, Dar