MTEMI: Chama Anajua Sana ila Aziz Hatari zaidi!



SIMBA inashuka uwanjani leo kuvaana na Orlando Pirates katika mechi ya kwanza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, bila ya kiungo wake mahiri, Clatous Chama anayebanwa na kanuni za michuano ya CAF.

Chama aliichezea RS Berkane katika mechi za awali za michuano hiyo na hivyo kutoitumikia Simba, lakini hilo halijamfanya nyota wa zamani wa klabu hiyo, Mtemi Ramadhani kumchambua Mzambia huyo, akidai ni fundi kwelikweli.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba aliyewatungua Al Ahly katika Kombe la Washindi (sasa Kombe la Shirikisho), amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi.

Ameelezea safari yake kisoka hadi alipostaafu na kukumbushia bao lake lililosaidia kuiua Al Ahly jijini Mwanza 1985, Simba ilipowaua Wamisri kwa mabao 2-1 na kutaja vikosi vyake vikali akiwachomoa nyota wanne wa Yanga. Mkongwe huyo aliizungumzia Yanga na kueleza miujiza pekee ndiyo inayoweza kuinyima ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, sambamba na mtazamo wake juu ya nyota wa kigeni katika timu za Ligi Kuu Bara. Endelea naye...!


CHAMA HATARI

Mtemi aliyewahi kukipiga Waziri Mkuu ya Dodoma kabla ya kutua Simba mwishoni mwa 1970, anasema Chama ni bonge la fundi.

Anasema kwa sasa nchini hakuna mchezaji mwenye uwezo kama Chama kwani anajua mpira na anajua timu inataka nini na kwa wakati upi, hivyo hata kukosekana kwake kwenye mechi za kimataifa ni pigo flani Simba.

“Chama anajua apige mpira kwa uzito upi. Unajua huu mpira mtu anaweza akakupigia ukashindwa kutuliza, lakini Chama ana makisio sahihi ya pasi pamoja na kotroo ya kuwango cha juu mno,” anasema Mtemi.


“Namzimia mno na nawaambia wale wanaosajili kutafuta wachezaji kama Chama yule anakupa kila kitu na ile kauli ya mchezaji wa kulipwa inakuja kwa vitendo kwamba ni lazima awe na uwezo kuliko wachezaji wa ndani hii inapatikana kwa Chama.”

ANDAMBWILE KAMA YEYE

Mtemi anasema mbali na Chama, kwa kuwaangalia viungo wakabaji waliopo, kiungo wa Mbeya City, Aziz Andambwile aliyewahi kukipiga Nyasa Big Bullets ya Malawi ni mchezaji mzuri na ni hazina kwa Taifa kutokana na kuwa na utulivu mkubwa anapokuwa na mpira.

Andambwile aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Taifa Stars na kufanikiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Sudan na Afrika ya Kati, na Mtemi anasema: “Kwanza ana urefu mzuri, hana mambo mengi na ukitaka udumu katika soka usiwe na pancha za mara kwa mara na kutokukaa na mpira ndicho anachofanya kijana yule. Ni hazina kwa Taifa nampenda sana na napenda kumwangalia. Naamini atakuja kuwa hazina kwa Taifa hili, akicheza najiona mimi kabisa.”

WAZAWA WANAWEZA

Anasema kumekuwa na kasumba ya timu kubwa nchini kutafuta makocha kutoka nje ya nchi ambapo Mtemi anadai si sahihi kwani kuna baadhi wana uwezo mkubwa.


Anasema wakati wanacheza wao kulikuwa na makocha wazawa walioaminiwa akitoa mfano Joel Bendera, Mohammed Msomali na walikuwa wakizipa matokeo timu zao.

Mtemi anashauri makocha wa sasa wapelekwe kusoma zaidi nje ya nchi ili wakirudi warudi na maarifa makubwa zaidi. “Kina Mkwasa (Charles) na yule Malale (Hamsini) ni wazuri sana na timu zao zinacheza vizuri, wakasomeshwe zaidi ili wakija waje na maarifa makubwa, hii itakuwa njia nzuri. Mimi naona kama vile hizi klabu kubwa zinaigana tu kutafuta makocha nje,” anasema.

KIM NA STARS

Anasema Kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen ni mtu makini, mnyenyekevu na anayesikiliza ushauri wa kila mtu na kubwa zaidi ni jinsi anavyowapa nafasi vijana.

Mtemi anasema ukiamini katika vijana kufanikiwa hakupo mbali kwani ni suala la kuwapa mbinu sahihi na kuwajengea kujiamini.


“Kuna wale vijana wanaocheza soka nje mfano Novatus Dismas na hawa wa hapahapa nyumbani wale wame-aminiwa na mwalimu Kim na hawakumwangusha lile ni jambo zuri sana,” anasema.

ALIA NA WAAMUZI

Mtemi anasema Ligi Kuu ina mvuto kutokana na kuonyeshwa na runinga, hivyo Watanzania wanapata nafasi ya kuangalia, hata hivyo bado kuna kasoro ambazo zimekuwa zikionyeshwa na waamuzi wanaochezesha michezo hiyo ikiwemo kutotafsiri kwa ufasaha sheria.

“Kitu kidogo wanapuliza filimbi. Filimbi zimekuwa nyingi mpaka inafika dakika za kucheza uwanjani zinakuwa chache, hili linaniudhi sana. Acha watu wacheze hii inampa faida yule ambaye amezidiwa kupoteza muda,” anasema.

Anashauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutafuta waamuzi watakaoondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza na hivyo kupoteza ladha ya mchezo.

WANNE TU YANGA

Mtemi anataja kikosi chake bora cha muda wote nchini enzi akiupiga kinachojumuisha wakali waliotamba 1970-1990.


Kikosi hicho ni Omary Mahadhi, Yusuf Ismail ‘Bana’, John Fire, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Mohammed ‘Adolf’ Rishard, Omary Hussein ‘Keegan’, Hussein Ngulungu, Peter Tino, Thuweni Ally na Celestine Mbunga ‘Sikinde’.

Kwa kikosi cha sasa, Mtemi aliweka ushabiki pembeni na kuwachomoa nyota wanne walipo Yanga akiwamo kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele aliyefunga 11, Farid Mussa na kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na pia yupo Bakar Mwamnyeto.

Mtemi pia aliwabeba nyota watatu wa Simba akiwamo kipa bora Aishi Manula, beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Chama na kikosi kizima kwa mtazamo wake ni hiki: Manula (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Tshabalala (Simba), Mwamnyeto (Yanga), Yakubu Mohamed (aliyekuwa Azam), Fei Toto (Yanga), Sakho (Simba), Chama (Simba), Mayele (Yanga), George Mpole (Geita Gold) na Farid Mussa (Yanga).

ANAFANYA NINI?

Mtemi anasema mara baada ya kustaafu soka amejikita zaidi katika kilimo kwani anaamini ndio sehemu sahihi.

“Sasa hivi nimepumzika najikita zaidi na kilimo. Mimi ni mkulima nalima Kiteto, nalima alizeti nimeona huko kuna fursa na maisha yanaendelea na namshukuru Mungu,” anasema.

AMEIZUNGUKA DUNIA

Kiungo huyo wa zamani anasema miongoni mwa faida aliizopata kutokana na soka ni kuizunguka dunia wakati akicheza.

“Kila inapocheza Stars lazima niende, fainali za Kombe la Dunia mara nyingi nimeenda kuziona. Kwa hili namshukuru Mungu. Mimi napenda mpira na mpira ndio maisha yangu, pia napenda timu inayocheza vizuri,” anasema.

Anasema kupitia mpira wakati huo alijenga nyumba na kuongeza uhusiano na watu mbalimbali.

TUKIO LA KUFURAHISHA

Mtemi anasema katika kusakata kabumbu amekutana na matukio mengi ya kufurahisha, lakini kubwa ni msimu wa Ligi Daraja la Kwanza wakati huo 1981 ambapo timu yake ya Simba ilicheza mechi zote za msimu bila kufungwa hata moja. “Kuna mechi hadi mapumziko tulikuwa tumefungwa tatu bila, tulipambana mpaka tukasawazisha magoli yote... ulikuwa ni msimu mzuri kwangu na kwetu na nilicheza mechi karibia zote,” anasema.

TUKIO LA KUHUZUNISHA

Mtemi anasema licha ya kucheza michezo mingi, lakini kwake kupewa kadi nyekundu ilikuwa ni nadra sana kutokana na kucheza kwa kutumia akili nyingi.

Anasema 1979 wakati akiichezea Waziri Mkuu katika mchezo dhidi ya Majimaji mwa- muzi

alimtoa nje kwa kadi nyekundu.

“Sikufanya kosa lolote hata mashabiki walishangaa kwanini nimepewa ile kadi, nilisikitika na ni tukio ambalo linabaki kuwa la huzuni kwangu kwa sababu katika maisha yangu ile ndio ilikuwa kadi ya kwanza na ya mwisho.”

WA KIGENI

Mtemi anasema ili ligi ya Bongo iwe bora ni lazima idadi ya wachezaji wa kigeni iangaliwe na wawe wenye uwezo mkubwa.

“Naona ikiwezekana ipunguzwe angalia wale Al Ahly wanachukua wachezaji we-nye uwezo mku-bwa kushinda wale wa kwao, sasa hapa kwetu wengine wanazidiwa uwezo na wazawa, hili hapana liangaliwe,” anasema.

Anashauri timu ziwe na wasaka vipaji watakaosaidia kujua wachezaji sahihi walipo kuanzia ndani ya nchi hadi nje.

WAWEKEZAJI WAJE

Mtemi anasema soka limebadilika na linahitaji fedha nyingi, hivyo mabadiliko ya mifumo yanahitajika ili kuwekeza kuanzia katika vifaa, miundombinu na usajili. “Ila nitoe angalizo wale wanaowekeza ni lazima wawe na nia njema ya kuendeleza michezo. Soka linahitaji uwekezaji mkubwa mno mno,” anasema.

AKIKUTANA NA RAIS

Mtemi anasema kama akifanikiwa kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan atamshauri kuongeza bajeti katika michezo na Serikali ihudumie timu zote za Taifa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Zamani hata mimi wakati naenda kuripoti kambini katika timu ya Taifa nilikuwa naenda kwa mtu wa Serikali ananiandikia gharama zangu zote kama ni ndege ama basi, fedha zilikuwa zikilipwa na Serikali, nikikutana na Rais nitamwomba aipunguzie mzigo TFF kwenye hizi timu za Taifa,” anasema.

“Mfano Mgonja (waziri wa zamani) wakati huo aliwahi kwenda Ujerumani kutafuta vifaa vya timu kit nzima kwa ajili ya timu ya Taifa na Serikali ndio iligharamia, tusingoje Afcon ndio kuwe na kamati saidia Taifa Stars ishinde.”

UCHAGUZI WA SIMBA

Anasema aliamua kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa bodi ya Simba kutokana na kuona anafaa kwani ameitumikia timu hiyo kwa mafanikio makubwa.

“Nilijikuta naingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Simba lakini baadaye nikabadilishiwa majukumu ya kazi, muda mwingi nikatakiwa kuwa Dodoma, hivyo isingewezekana, haya mambo ni wito usilete tamaa siwezi kukaa Dodoma nikafanya kazi vizuri,” amesema.

LENNY ALIKUWA ANAJUA

Anasema wakati akicheza kulikuwa na wachezaji wengi wenye vipaji vya kusakata kabumbu, lakini Hayati Ramadhan Leny alikuwa ni zaidi ya wote.

“Nimekutana na wachezaji wengi, lakini Leny alikuwa anajua sana mpira, alikuwa fundi aliyekamilika, muda mwingi unatamani kumuona jinsi ambavyo alikuwa akicheza. Anayefuata ni Adolf Richard.”

AWACHANA MASTAA WA SASA

Kuhusu mastaa wa sasa, mkongwe huyo anasema: “Nawashauri wafanye mazoezi wachezaji wengi wamekuwa wavivu na timu nyingi hazifanyi mazoezi, hivyo mchezaji lazima uwe na ratiba yako binafsi ili kujiweka fiti.

“Ushauri wangu mwingine ni nidhamu, wawe na nidhamu hawawezi kufanikiwa kama huna nidhamu hata kwenye maisha ya kawaida,” anasema.

ATIA WINO TIMU TATU

Katika simulizi yake, Mtemi anasema baada ya Afcon alikumbana na kifungo cha mwaka mmoja kutokana na kusajiliwa timu tatu katika msimu mmoja ambazo ni Pan African, Yanga na Simba.

“Pan ndio walianza kunifuata tukakubaliana wakanisajili, lakini baada ya kumalizana na Pan, Yanga nao wakaja wakanishawishi nijiunge nao tukakubaliana wakairejeshea Pan fedha yao. Nataka kujiunga na Yanga, Simba nao si wakaja wakanishawishi niachane na Yanga nijiunge nao. Kiukweli tangu utoto wangu nilikuwa naipenda sana Simba, sema ndio vile nisingeweza kujipeleka,” anasema.

“Hivyo walivyonifuata wala sikujivunga wakaahidi kuwarejeshea Yanga fedha yao waliyonipa, hapo ndipo kimbembe kilianzia mwishowe nikafungiwa kujihusisha na soka mwaka mmoja hadi 1981.”

USAJILI WANUNUA KITANDA

Mtemi anasema fedha yake ya kwanza ya usajili ilikuwa Sh17,000 na aliipata baada ya kujiunga na Simba akitokea Waziri Mkuu ya Dodoma 1979.

“Nilienda moja kwa moja kununua kitanda, makochi, haikuwa fedha kubwa, lakini kwa kipindi kile ilikuwa na thamani kubwa,” anasema.

ALIVYOITUNGUA AL ALHY

Mtemi akiwa Simba anakumbuka 1985 walicheza na Al Ahly ya Misri jijini Mwanza mechi waliyoamini watafungwa nyingi, lakini wakawaduwaza Wamisri kwa kuwapa kipigo cha mabao 2-1 moja akitupia mwenyewe kambani.

“Hii inabaki kuwa mechi yenye thamani kuliko zote katika maisha yangu, nilipokea pasi kutoka kwa Zamoyoni Mogella na kutuliza na mguu wa kulia na kisha kupiga shuti kwa mguu wa kushoto. Sio kawaida kwangu kutumia mguu wa kushoto, lakini nilifunga,” anasema.

“Wakati ule Al Ahly walikuwa bora kwelikweli achana na hii timu ya sasa. Bila shaka ndio walikuja kuwa mabingwa wa Afrika wakati ule. Wengi walijua tutapoteza, lakini tuliwanyoosha Kirumba bila wenyewe kutarajia.”

Anasema yeye na Mogella ndio waliofunga akianza Mogella kabla ya yeye kufunga bao la ushindi, japo Simba ilipoteza ugenini 2-0 na kutolewa mashindanoni.

Mtemi anasema, baada ya kurejea kutoka Misri aliendelea kucheza lakini sio kwa kujitoa kutokana na majukumu ya chuo. “Tuliporejea nchini nilikuta jina langu ni miongoni mwa yaliyochaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu, hivyo muda mwingi niliutumia masomoni, sikujihusisha sana na mpira. Muda ulikuwa mchache sababu kuna wakati natakiwa nifanye kazi za chuo, ndipo muda ambao pia natakiwa niwepo kwenye mazoezi au mechi za Simba, nilishindwa kujigawa.”

MECHI ASIYOISAHAU

“Ilikuwa katika Afcon 1980 dhidi ya Misri mpaka karibia na jioni tulikuwa 1-1 dakika za mwisho kabisa Tenga alifanya makosa jamaa wakapata bao la pili niliumia sana kwani tulikuwa nafasi nzuri.

“Mechi nyingine dhidi ya Ivory Coastal tulitoka 1-1 na dhidi ya Nigeria tulifungwa 3-1 kipindi kile tulikuwa na timu yenye ushindani sana angalia majina hayo tuliyokutana nayo,” anasema.

HISTORIA

Mtemi Ramadhani alizaliwa Novemba 25, 1956 jijini Dodoma, alipata elimu yake ya msingi Rugambwa kuanzia 1962-1968, kisha alijiunga na Sekondari ya Dodoma (1969-1972) na baadaye kujiunga na Chuo cha Ushirika Moshi (1965-1975), kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1985-1988) alikochukua Shahada ya Kwanza ya Biashara.

Mkongwe huyo alianza kucheza soka JKT Makutupora ya Dodoma kisha Waziri Mkuu na Simba, na aliitumikia timu ya Taifa kwa miaka saba akiwamo katika kikosi kilichofuzu fainali za Kombe la Afrika (Afcon) 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.



Kuwa wa kwanza kutoa maoni

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad