SalimAziz Mkurugenzi wa Kamouni ya Uzalishaji wa Bidhaa za Vyakula ya Bakhresa
MTANZANIA Salim Aziz ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi wenye umri mdogo nchini Tanzania akitokea Kampuni ya Bakhresa Group, amefanya mahojiano na Kituo cha Runinga cha CNN cha Marekani na kuelezea masuala mbalimbali ya uchumi wa Tanzania, ikiwemo jinsi reli ya kisasa ya SGR itakavyofungua uchumi wa Tanzania.
Akizungumza katika mahojiano hayo, Salim ambaye amekuwa na uzoefu wa kutosha katika shughuli za uzalishaji pamoja na usimamizi wa biashara, amesema kuanza kufanya kazi kwa reli hiyo kutarahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zikiwemo Rwanda na Uganda na kuongeza idadi ya mizigo itakayokuwa inapitia katika Bandari ya Dar es Salaam.
Salim Azizi akiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
“Itatusaidia sana kama taifa lakini pia itatusaidia kama mwananchi mmojammoja, naamini fursa nyingi za ajira zitafunguka kwa vijana na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi,” alisema Salim ambaye pia ni mhitimu wa Shahada ya kwanza ya Masomo ya Biashara pamoja na Udhibiti wa Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Salford cha nchini Uingereza.