Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Omary Mugisha mfanyabiashara katika Soko la Mwenge Jijini Dar es Salaam amekutwa leo Aprili 13, 2022 majira ya asubuhi akiwa amenasa juu ya paa la nyumba lililokuwa na umeme huku akiwa amefariki.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhani Kingai amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu ametambulika kuwa ni Omary Mugisha, Muhaya mwenye umri wa miaka 42 na mkazi wa Mwanagati Jijini Dar es salaam aliyekuwa mfanyabiashara katika soko la Mwenge.
ACP Kingai, amesema kwamba mtu huyo alikuwa akijaribu kujiunganishia umeme na kwamba pembeni yake kulikuwa na kifaa cha kukatia nyaya pamoja na waya wa umeme huku akiwa ameshikilia bisibisi.
"Ni kweli huyo Bwana alikutwa kwenye paa la nyumba akiwa amefariki kwa kupigwa na shoti ya umeme, ni kwamba alikuwa akijiunganishia umeme katika kibanda chake. Hakua na vifaa kinga kama gloves, lakini tumemkuta akiwa na waya pamoja na pisipisi mkononi. Mwili wake umehifadhiwa hospitali ya Mwananyamala kwa utambuzi" - ACP. Kingai, RPC Kinondoni.
Kwa upande wake M/kiti wa mtaa wa Mwenge, Bashir Hozza amesema kuwa marehemu alikuwa akijaribu kujiunganishia umeme kiholela usiku katika kibanda chake.
"Huyu Bwana alikuwa anajiunganishia umeme na hii ni kazi ambayo amekuwa akiifanya kinyume cha sheria. Kwahiyo kama mlivyoona huyu ni mzembe. Alipanda bila hata tahadhari, hana gloves, hana viatu na mvua ilivyokuwa imenyesha akanaswa na umeme" - Bashir Hozza, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mwenge.
Aidha, mashuhuda na watu waliobaini tukio hilo awali wamesema kuwa marehemu alikuwa ni fundi wa umeme katika eneo hilo.
"Huyu Omary tunamfahamu anakibanda hapa, na ni fundi wetu wa umeme hapa, huwa anatutengenezea umeme lakini hatujui kama huwa anavyeti au hana. Ndo hivo imetokea amepigwa shoti" - Mama Willy, Mfanyabiashara Mwenge.