INAELEZWA bondia namba moja Tanzania, Hassan Mwakinyo amefanikiwa kusaini mkataba wa kucheza ngumi nchini Marekani wenye thamani ya Sh milioni 232 chini ya bondia wa zamani na promota Dmitriy Salita wa Kampuni ya Salita Promotion.
Mtanzania huyo ambaye kwa sasa anaishi na kufanya mazoezi nchini Marekani amevuliwa ubingwa wa Afrika ABU ikiwa imepita miezi kaadha tangu Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani ‘WBF’ kumvua mkanda wake wa ubingwa wa Dunia wa WBF.
Taarifa za kuaminika kutoka kwa watu wake wa karibu, wamekiri kuwa moja ya jambo linampa kiburi kwa sasa bondia huyo ni baada ya kufanikiwa kusaini mkataba na Kampuni hiyo ya Salita Promotion chini ya Mmarekani Salita mwenye asili ya Ukraine.
“Tatizo watu wengi wanashindwa kumuelewa Mwakinyo nini ambacho kwa sasa anakilenga katika ngumi maana ndiyo kazi yake hivyo kitendo cha yeye kupoteza mikanda ya ubingwa wa WBF na ABU kwake imekuwa ni jambo la kawaida kwa sababu amesaini mkataba na promota mkubwa nchini Marekani anaitwa Dmitriy Salita ambaye zamani alikuwa bondia.
“Mkataba aliosaini unafika milioni 232 japo kuwa bado wenyewe wamekuwa wakifanya ni jambo la siri kwa kuwa baadhi ya mambo bado hayajakamilika lakini ni kwa sasa watu wasahau kuona Mwakinyo akicheza tena hapa nchini kwa kuwa anataka kupigania mkanda mikubwa ya ubingwa,” alisema mtoa taarifa.
Championi lilimtafuta Mwakinyo ambaye alisema: “Ni kweli nimesaini mkataba ila muda wa kuweka wazi ukifika basi nitakwambia kila kitu ila kwa sasa nimekuwa nikiendelea kujifua hapa Marekani maana malengo yangu ni kupigana katika kuwania mikanda mikubwa na mabondia wa kubwa.”
Stori na Ibrahim Mussa