Mwanamke Aliyeolewa na Roho Mtakatifu Azikwa Usiku Baada ya Mwili Wake Kupatikana Kichakani




Marehemu Elizabeth Nalem ambaye alifunga ndoa na Roho Mtakatifu mwaka jana
Mwanamke 'aliyefunga ndoa' na Roho Mtakatifu mwaka jana alizikwa usiku mapema wiki hii baada ya kupatikana amefariki katika msitu wa mmoja wa Pokot Magharibi.

Mwili wa Elizabeth Nalem, 42, ulipatikana siku ya Jumamosi na mvulana aliyekuwa anafuga.

Mama huyo wa watoto sita aligonga vichwa vya habari mwaka jana baada ya kuachana na mumewe, kufunga hoteli yake na kuamua kufunga ndoa na Roho Mtakatifu huku akiwa amevalia gauni jeupe.


Kulikuwa na shamrashamra kubwa wakati wa harusi na umati mkubwa ulishuhudia tukio hilo la kushangaza..

Mwanamke huyo alisema Roho Mtakatifu alimwelekeza akahubiri injili na akadai angepewa ndege aina ya chopa.

Joshua Nalem alithibitisha kuwa alimzika mkewe usiku wa Jumatatu kwa kuwa hawakuwa na lingine la kufanya.

Familia ilisema marehemu alikuwa amekosekana kwa wiki tatu.


Nalem alisema walipiga ripoti kwamba mkewe amepotea huku wakiendelea kumtafuta.

"Tuliishi kwa amani baada yake kurudi nyumbani baada ya harusi," alisema.

“Niliposikia mwili wa mwanamke umepatikana, niliamua kwenda kuuona. Hapa ndipo nilipomaliza msako mrefu wa kumtafuta mke wangu. Nilithibitisha ni yeye kwa vile mkoba wake ulikuwa kando ya mwili wake,” alisema.

Nalem alisema siku ambayo mkewe aliondoka nyumbani, aliacha simu yake na Biblia.


"Alikuwa akitoka nyumbani na kwenda misheni lakini alikuwa anarudi. Wakati huu hata hivyo, hakuwahi kurudi. Ndiyo maana tulimripoti kama mtu aliyepotea," alisema.

OCDP wa Kapenguria, Kipkemoi Kirui alisema uchunguzi wa maiti haukutekelezwa.

"Familia na mume wa marehemu walitia saini kwenye hati ya kiapo mbele ya polisi baada ya kukataa uchunguzi wa maiti," alisema.

Kirui alisema polisi wanaendelea kufuatilia kisa hicho na iwapo watapata mchezo wowote mchafu, mwili huo utafukuliwa.

Mwaka jana baada ya harusi yake, mwanamke huyo alisema kwamba Mungu alikuwa amemtuma kuhubiri injili. Ndiyo maana alifunga biashara yake ya hoteli kwani ingeweza kukatiza mwito wake mpya.


Mwanamke huyo alisema Roho Mtakatifu alimwambia atapewa chopa ili kusaidia kueneza neno la Mungu ulimwenguni.

Nalem alisema aliagizwa kuanza kazi yake katika eneo la Amudat, nchini Uganda lakini alitakiwa kurudi nyumbani kwanza.

"Nilipangwa kuanza kuhubiri neno la Mungu huko Amudat lakini niliombwa kurudi nyumbani na kuhakikisha amani imepatikana kabla ya kuelekea nchi jirani," alisema.

Alimhakikishia mume wake na watoto kwamba hajawaacha bali wanapaswa kumruhusu afanye mapenzi ya Mungu.

"Kazi hii haihitaji vikwazo. Ndiyo maana naiomba familia yangu ipumzike kwani nitakuwa nikieneza Neno na kurudi kwao,” alisema

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad