MZEE WA UPUPU: Sio muda sahihi haya kutokea ndani ya Simba



WAKATI wowote kuanziaa sasa kocha mkuu wa Simba, Pablo Franco Martinez anaweza kuondoka klabuni hapo. Ambacho hakijulikani ni kimoja tu, ataondoka kwa kufukuzwa kama kina Uchebe au kwa kuacha kazi mwenyewe kama Sven.

Hii ni kutokana na kinachodaiwa kuwa suala la uhusiano wa kikazi. Hali hii inadaiwa kuwapo kwa muda mrefu, lakini kwa sasa inaelezwa kuwa ni mbaya hasa kutokana na pengo la alama kutoka vinara wa Ligi Kuu, Yanga na wao kama mabingwa watetezi.

Baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union pale Mwakwani Tanga, Simba ilienda Moshi kucheza na Polisi Tanzania. Wakiwa hapo Pablo akakataa kufanya mazoezi na kikosi chake kwa sababu uwanja waliotakiwa kuutumia haukuwa na kiwango ambacho yeye anataka. Kwa hiyo timu iko uwanjani lakini mazoezi hayafanyiki, kocha hataki.

Ikabidi meneja wa timu apige simu kwa kigogo mmoja kumuelezea kinachoendelea. Kigogo huyo akampigia simu Pablo, hakupokea. Akampigia meneja ili ampe simu Pablo waongee, Pablo akakataa kuongea. Akampigia simu kocha msaidizi, akaongea naye kwa dakika kadhaa, simu ikawa ya moto. Kocha msaidizi akaja na simu kwa Pablo ili aongee na bosi Dar es Salaam, akakataa kuchukua simu.


 
Kocha msaidizi akaenda tena pembeni, akaongea naye kwa dakika kadhaa halafu akarudi. Akapiga filimbi kuwaita wachezaji uwanjani. Inavyoonekana bosi alisema kama kocha hataki wewe simamia mazoezi. Mazoezi yakaanza na baadaye Pablo akaungana na wenzake hadi mwisho.

Siku ya mechi Pablo akawapumzisha wachezaji muhimu waliozoeleka akihofia kuwachosha au kuwaumiza kuelekea mchezo wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates. Mechi ikaisha kwa sare tasa na kumkera sana kigogo huyo akiamini ingewezekana kupata ushindi endapo kocha angepanga nyota wake wote.

Waliporudi Dar es Salaam malumbano kati ya kocha na bosi wake yakaendelea kiasi cha kocha huyo raia wa Hispania kujibu, ‘niandikie barua ya kunifukiza nije niisaini halafu tukutane aidha kwenye nusu fainali au fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika.’


Pablo alimaanisha kwamba kuna timu zinamtaka ambazo zipo kwenye hatua ya robo fainali, hivyo akiondoka tu Simba hakai muda mrefu atatangaza sehemu nyingine na kama mambo yataenda sawa atakutana na Simba. Mgogoro kama huu ulitokea kwa Sven walipokuwa Zimbabwe kwenye mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum.Wakiwa mazoezini, Sven aliwafukuza waandishi wa habari, viongozi wa timu na hadi maofisa wa ubalozi wa Tanzania. Tabia ya Sven kufukuza watu mazoezini ilikithiri pale alipowafukuza wajumbe wa bodi ya klabu. Wajumbe walikuwa na kikao chao na baada ya kikao hicho wakataka waangalie mazoezi kidogo pale Bunju.

Lakini wakashangaa mazoezi hayaanzi hadi walipouliza na kuambiwa kocha hataki kuanza mazoezi hadi muondoke, na kweli wakaondoka. Misuguano ya aina hii ikawa mikubwa na wakaanza kuviziana, lakini Sven akawawahi na kuacha kazi.

Sasa mambo yamegeukia kwa Pablo, misuguano ya chini kwa chini imeanza siku nyingi lakini kwa sasa hali ni mbaya. Itakuwa busara sana kwa wakubwa wa klabu wakalitambua hili na kulishughilikia mapema kabla mambo hayajaharibika. Huu siyo muda sahihi wa haya kutokea ndani ya Simba.

Inahitajika amani ili kuleta umoja utakaoisaidia timu kufanya vizuri katika mchezo wa mkondo wa pili kule Afrika Kusini.


 
Historia inaonyesha kwamba Simba hupata tabu sana katika mechi za ugenini katika hatua kama hii.

Na kwa namna wakivyocheza Orlando Pirates na hasira alizozionyesha baada ya mechi kupitia kocha wao kwenye mkutano na waandishi wa habari, ina maana Simba watakutana na wakati ngumu sana kule Soweto. Bila amani umoja na mshikamano, hakuna nafasi kwa Simba kutoboa.Litakuwa pigo kubwa sana kwa Simba na Tanzania kuona kwa mara ya tatu katika miaka mitano, Simba wanashindwa kuvuka hatua hii. Ni matumani yangu kwamba Simba ina watu wenye busara, waitumie sasa kutuliza mambo.

Ni mimi mzee wa Upupu.


Kuwa wa kwanza kutoa maoni


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad