Pablo awapongeza wachezaji wake



Pablo awapongeza wachezaji wake
KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco amewasifu wachezaji wake kwa kujituma muda wote wa mchezo licha ya kutolewa katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Orlando Pirates kwa penalti 4-3.

Katika mchezo huo, Simba ilifungwa 1-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1 baada ya Wekundu hao wa Msimbazi nao kushinda 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na hivyo kupigiana penalti ili kumpata mshindi.

Pablo alisema kuwa amefurahishwa na jinsi wachezaji wake walivyojituma na kujitahidi kufuata maelekezo, kitu ambacho anajivunia.

“Nawapongeza sana wachezaji wangu kwa moyo wa kujitolea kwa ajili ya timu licha ya kucheza pungufu uwanjani muda mrefu. Mchezo ulikuwa mgumu na wakuvutia, lakini tutasubiri kwa mwaka mmoja kufikia malengo yetu.


 
“Siku zote penalti hazina mwenyewe ila nilichopenda ni jinsi wachezaji wangu walivyopambana. Pia niwapongeze Orlando walikuwa bora ndani ya dakika 90, sisi safari yetu imeishia hapa tutajipanga mwakani,” alisema Pablo.

Alisema Orlando walikuwa bora zaidi yao katika dakika 90, walicheza vizuri kuliko wao, lakini anajivunia timu yake jinsi ilivyopambana kwa mara ya kwanza ameshuhudia Simba ikicheza mchezo mgumu ugenini kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho.

 “Nakumbuka tulicheza wote tukiwa 11 uwanjani, Orlando hawakupata bao na walikuwa na mchezaji mwenye mabao mengi kwenye michuano hii katika hatua ya makundi, lazima tuongeze thamani yetu.”


“Nafikiri kama tusingekosa mchezaji mmoja ungekuwa mchezo mgumu kucheza na pengo la mtu mmoja linafanya mtu kulinda watu wawili na  kwenye penalti, kuna hitaji ubora na uchambuzi, lakini pia inahitajika bahati, tulikuwa karibu kuingia nusu fainali tunajipanga kwa ajili ya msimu ujao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa,” alisema Pablo.

Kocha Mkuu wa Orlando Pirates, Mandla Ncikazi, alisema kuwa aliingia kwenye mchezo huo akiwa na tahadhari sana ndio sababu aliwaacha nje baadhi ya wachezaji wake muhimu kama Gabadinho Mhango, Dlamin na Mabasa ili waweze kuusoma mchezo na kwenda kuuamua.

“Simba waliingia na staili ya kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza hilo walifanikiwa kipindi cha kwanza, tuliporudi vyumbani niliwaambia vijana wangu waongeze nguvu ya kutengeneza mashambulizi, hasa kwa mipira ya krosi ambao mmoja alifunga bao,” alisema.

Alisema kuwa Simba walikuwa bora sana, walicheza kwa tahadhari lakini penalti zimewapeleka hadi nusu fainali, hivyo wanasahau yaliyopita wanaangalia wataingiaje kuwakabili Al Ittihad ya Libya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad