‘Panya Road’ Gumzo Kubwa Dar..Majeruhi Wasimulia

 


Wakati vijana kumi wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za uvamizi wa nyumba tofauti Chanika jijini hapa, majeruhi katika tukio hilo wamesimulia njia zilizotumiwa na wahusika hao kutekeleza uhalifu huo

Watuhumiwa hao maarufu kwa jina la ‘Panya Road’ walidaiwa kusababisha taharuki na kujeruhi watu 23 waishio Chanika, huku wakipora vitu mbalimbali ikiwamo fedha, simu na runinga.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, majeruhi walidai watuhumiwa hao walipokuwa wakitekeleza uhalifu huo, walitumia mbinu ya kufika nje ya nyumba na kupiga mayowe ya kuita mwizi, ili kushawishi watu kutoka nje ya nyumba zao kutoa msaada na walipofanya hivyo walishambuliwa.

“Wakati wanafika kwangu saa 9:20 usiku nilikuwa sina muda mrefu tangu nilale, nilikuwa na usingizi hasa, zile kelele za mwizi na kishindo kilichokuwa kikisikika wakati wanavunja mlango kilimfanya kaka yangu atoke ndani kwenda kuangalia ni nini kinaendelea,” alisema Rashid Jumbe.

Alisema kaka yake alipofungua mlango wa nyuma alishtuka kuona kundi kubwa la vijana wakiwa na mapanga mikononi, jambo lililomfanya kurudi ndani kujiokoa.

“Wakati anarudi ndani, tayari mlango wa mbele umevunjwa na kitu kizito na watu wenye mapanga wameingia, ikabidi arudi tena mlango wa nyuma akimbie akiwa na nguo ya ndani pekee, wengine wakaanza kumkimbiza huku wakimuitia mwizi na wengine wakabaki hapa ndani,” alisema Jumbe.

“Mlango wa chumbani kwangu waliingia na teke moja wakaanza kunishambulia kwa mapanga na walibeba simu mbili kwa kuwa niliwaambia sina hela.”

Wakati hayo yakiendelea, mpangaji wake aliyejaribu kutoka nje ili kusaidia hakufanikiwa kwa kuwa baada ya kufungua mlango na kuona vijana wengi wenye mapanga aliamua kurudi ndani na alipojaribu kufunga mlango alikuwa amechelewa hivyo walianza kusukumana.

“Wakati yeye (mpangaji) akisukuma nje afunge mlango, na wao walisukuma ndani waufungue, mmoja wao akasema muacheni huyu tukivunja tukiingia tunamuua, aliogopa akafungua mlango, wakamjeruhi kwa mapanga na kuchukua Sh60,000 alizokuwa ameweka mezani,” alisema Jumbe.

Kabla ya kufika nyumbani kwa Jumbe watu hao walianzia kwa Joyce Sanga na mumewe ambako hawakufanikiwa kupata chochote baada ya kuhangaika kuvunja geti la mlangoni kwa zaidi ya nusu saa bila mafanikio.

Baada ya kushindwa kuvunja geti hilo waliamua kumalizia hasira zao kwa kuvunja vioo vya madirishani.

“Wakati huo wote tulijificha maana lolote lingeweza kutokea, jirani yetu aliyekuwa akisikia kelele za mwizi alitoka kuja kusaidia, bahati mbaya akakatwa mapanga sehemu tofauti za mwili,” alisema Joyce.

Alisema wakati tukio likiendelea, walihangaika kupiga simu polisi bila mafaniko na polisi walipofika, tayari uhalifu ulikuwa umetendeka, hivyo waliishia kupeleka majeruhi hospitalini.

Wakati baadhi ya nyumba akijeruhiwa mmoja mmoja, nyumba ya Mariam Hassan ni tofauti kwasababu wamejeruhiwa vijana watatu.

Kwa sasa anauguza vijana wake wenye majeraha sehemu tofauti za mwili walioshumbuliwa na kundi hilo.


Akiwa bado na hofu moyoni kutokana na shambulio hilo ndani ya familia yake, lakini hajui ni namna gani atawatibu vijana wake, Khamis Kessy na Salum Said wanaohitaji Sh1 milioni na Sh600,000 mtawaliwa baada ya kujeruhiwa.

Kessy ambaye ni mtoto wa mwisho wa mama huyo alikatwa mapanga mara nane sehemu tofauti za mwili, ikiwamo manne kichwani aliposhonwa huku akivunjwa mkono.

Salumu alipigwa na kitu kizito katika goti kilichofanya mguu kugeuka na ili kufanyiwa upasuaji Sh600,000 zinahitajika, huku Maonesho Nassor yeye akijeruhiwa shavuni karibu na jicho kwa panga sehemu ambako ameshonwa.

“Mimi sina kazi yoyote kwa sasa ninayofanya, nilikuwa nauza sambusa lakini baadaye nilifiwa na mdogo wangu mwanzoni mwa mwaka huu na matatizo mengine yalitokea yakaua biashara yangu, sijui nawatibiaje, naomba nisaidiwe,” alisema Mariam ambaye ni mzazi wa vijana hao.

Katika nyumba hiyo, vibaka waliambulia simu mbili pekee licha ya majeruhi watatu waliowaacha huku wengine wakihitaji pesa nyingi za matibabu.

Majeruhi wasimulia

Salum alisema walishambuliwa ikiwa ni muda mchache baada ya kusikia kelele za mwizi katika nyumba ya jirani, jambo lililowafanya kubana katika chumba kimoja kwa makini ili kuangalia kinachoendelea.

“Wakati tumeamua sasa kutoka katika kile chumba kila mtu akalale, tulipofika sebuleni tulishtushwa na kishindo kikubwa cha mlango kuvunjwa na watu kuingia ndani moja kwa moja na kuanza kutushambulia, nilipojaribu kujitetea nilipigwa na kitu kizito na mguu kugeuka, wakanibeba na kunitupa nje,” alisimulia Salum.

Tabata hali ikoje?

Wakati hayo yakitokea Chanika, eneo la Tabata nako hali haikuwa shwari baada ya kundi la vijana kuvamia baadhi ya maduka huku wakibeba fedha na kujeruhi baadhi ya watu.

“Ilikuwa saa 3:15 usiku, nilimtuma dada wa kazi duka la jirani na nyumbani, wakati yuko pale alizungukwa na vijana waliovamia duka hilo wakitaka pesa, dada alipigwa na ubapa wa panga akazimia huku vijana hao wakichukua pesa ndani ya duka hilo,” alisema mmoja wa waathirika ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Tukio hilo lilifanyika pia katika maduka ya jirani kwa kuingia na kuchukua fedha kabla ya kuendelea katika nyumba nyingine.

Simulizi hizo zimetolewa wakati ambao Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akiviambia vyombo vya habari kuwa vijana 10 waliokamatwa umri wao unaanzia miaka 13 hadi 21 wakidaiwa kuongozwa na Abdullahzizi Abdallah na wenzake tisa.

Alisema baada ya kuhojiwa vijana hao, wamekiri kuhusika na matukio hayo na wameendelea kulisaidia jeshi hilo kuhakikisha wenzao wanaotoka maeneo mbalimbali waliyohusika na matukio hayo wanakamatwa.

“Vijana hao wamekuwa wakitumia mapanga kuwajeruhi watu. Sisi Jeshi la Polisi tuliongea na wenyeviti wa mtaa na mabalozi tumekubaliana hali hiyo haiwezi kuendelea, lazima watapambana na mkono wa chuma vijana wanaojihusisha na matukio hayo,” alisema Muliro.

Alisema mbali na vijana hao kuiba mali za watu katika tukio hilo, Chanika waliwajeruhi watu 23 kwa kuwakata mapanga sehemu mbalimbali na wengi wao wapo hospitali wanakiendelea na matibabu huku wengine wakiruhusiwa kwenda nyumbani.

“Vijana hao ni wadogo wamekamatwa na wameongea mambo mengi, naamini kulingana na uchunguzi tunaoendelea kuufanya tutafika pazuri,” alisema Muliro.

Alisema alipata taarifa za vikundi vingine kufanya matukio hayo maeneo ya Tabata, huku akiwataka wananchi kuunda vikundi shirikishi na kwamba maeneo yote yenye vikundi hivyo hakuna matukio hayo.

“Maeneo ambayo yana vikundi shirikishi huwezi kusikia vikundi hivi vikipata fursa, kuna vijana kama saba walitaka kufanya matukio Chanika lakini wananchi walikuwa imara na walikimbizwa hadi msitu wa jeshi na kupotelea kusikojulikana,” alisema Muliro.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad