JESHI la Polisi mkoani Tabora linachunguza kubaini mafuvu na masalia ya miili ya binadamu iliyokutwa katika pori la Uyogo wilayani Urambo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Richard Abwao alisema mwili wa mtu ulikutwa kwenye eneo hilo na kwamba masalia ya miili na mifupa imepelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi.
Abwao alisema jeshi hilo linaendelea na msako kukamata watu waliofanya mauaji hayo na kuacha mabaki ya mifupa na mafuvu.
“Tunafanyia uchunguzi juu ya masalia hayo na kubaini ni nini chanzo cha mauaji hayo yaliyosababisha mtu au watu kutupwa katika pori la Uyogo na kuutupa mwili wa mtu ambaye jina lake halijafahamika ni nani na anatokea wapi kwenye maeneo ya Urambo,” alisema Kamanda Abwao.
Hivi karibuni, iliripotiwa taarifa juu ya kupatikana mafuvu ya watu katika pori lililopo Kata ya Uyogo.
Awali, wananchi walilalamikia upotevu wa ndugu zao na mmoja alibainika kupotea katika kitongoji cha Kitega Uchumi, Kata ya Urambo na baadaye masalia ya mwili na nguo zilitambuliwa na ndugu zake na kulazimika kumzika katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasela, Kata ya Uyogo, Tomas Petro alisema awali walibaini masalia ya watu waliokufa katika kisima kimoja kilichopo karibu na pori hilo ndipo jeshi la polisi lilifika kwa ajili ya hatua za kiusalama.