Polisi wapigwa butwaa kukamata gari inayojiendesha




Polisi wa San Francisco wamekumbana na tukio ambalo hawajawahi kuliona katika siku za karibuni baada ya ofisa mmoja kusimamisha gari lililokuwa halijawashwa taa usiku, na kukuta hakukuwa na mtu ndani yake.
Baadaye ilibainika, gari hilo lilikuwa likijiendesha na tukio hilo la polisi lilinaswa kwa video na mpita njia, ambaye aliituma kwenye mtandao wa kijamii.

Video hiyo, inayoonyesha maofisa wa polisi wakiwa na mshangao wakilizunguka gari na kuchungulia ndani kwa dakika kadhaa, imetumwa kwa watu wengi mtandaoni na kampuni inayolimiki, Cruise, iliamua kuzungumzia katika akaunti yake ya Twitter kuelezea kilichotokea.
Ilisema gari hilo linalojiendesha lilisogelea gari la polisi na baadaye kujiegesha katika eneo salama karibu yake kama ilivyotakiwa.
Katika video hiyo, wakati polisi wakilikagua, mtu mmoja anasikika akisema "hakuna mtu ndani, ajabu".

Msemaji wa polisi alisema baada ya polisi kulisimamisha gari, timu ya matengenezo ililichukua.
Cruise ilisema taa za gari hilo zilizimika kutokana na makosa ya kibinadamu.

Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2013 imetengeneza programu ya kompyuta ambayo inawezesha gari kujiendesha bila ya kuongozwa na mtu.

Kampuni kubwa ya kutengeneza magari nchini Marekani, General Motors, inamiliki sehemu kubwa ya hisa katika kampuni ya Cruise.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad