Raia wa China amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kuwatesa wafanyakazi kwenye mgodi nchini Rwanda baada ya video iliyomuonyesha akimchapa viboko mwanamume aliyekuwa amefungwa kwa kamba kwenye mti, kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Shjun Sun, meneja wa mgodi magharibi mwa Rwanda alitiwa hatiani Jumanne pamoja na mshirika wake baada ya kukamatwa mwezi Septemba mwaka jana.
“Ni wazi kuwa bwana Shjun aliwatesa waathirika kwa kuwachapa viboko kwa nia ya uovu, na hili ni kosa kubwa,” Jaji Jacques Kanyarugira aliamua, na kumuamuru kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Shjun, ambaye alikuwa mahakamani kusikiliza uamuzi wa mahakama dhidi yake, alikiri kuwanyanyasa wafanyakazi wawili, akisema aliwapiga kwa sababu alikuwa “na hasira na kuchoshwa na tabia yao ya kuiba madini mara kwa mara.”
Raia huyo wa China mwenye umri wa miaka 43 alijitetea aachiliwe huru, akisema kwamba aliwalipa wafanyakazi hao wawili fidia ya franka milioni 1 pesa za Rwanda, sawa na dola 1,000 za Marekani, na kusaini barua ya maridhiano.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ambao ulikuwa umemshtumu kwa kunyanyasa watu wanne, ulieleza kuwa waathirika walikubali malipo ya fidia “kwa sababu walikuwa wamechanganyikiwa na walikuwa wanamuogopa.”
Meneja mwingine wa kampuni ya Ali Group Holding Ltd, alikutwa na hatia ya kumsaidia Shjun na alihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela, lakini mshtakiwa mwingine alikutwa bila hatia.