Mwizi mmoja alijipata pabaya baada ya silaha yake kumgeuka na kumla alipojaribu kumvamia mtu mmoja eneo la Njiru, jijini Nairobi.
Kulingana na wapelelezi wa DCI, mwizi huyo alijaribu kumuibia jamaa mmoja raia wa Tanzania aliyekuwa ametembelea mpenzi wake wakati Mtanzania huyo alipomla chenga na kumnyang’anya bastola aliyokuwa akimtishia nayo na kisha kumshambulia nayo vikali.
DCI walieleza kwamba raia huyo wa Tanzania, Simon Sanga alikuwa ametembelea mpenzi wake maeneo hayo ambapo usiku wa manane walitoka kwa gari lao ili kuenda sehemu ya burudani kujivinjari.
Wapenzi hao wawili walipofika katika klabu moja ambapo walipata kwa bahati mbaya kumefungwa. Hapo ndipo Sanga aliamuaga mpenziwe ndani ya gari na kuamua kutoka nje ya gari ili kujaribu kuangalia kama wahudumu wa baa ile wangeweza kuwafungulia ili kujivinjari pale kwa vileo.
Pindi tu Sanga alipokuwa amekaribia mlango wa baa ile, pikipiki iliyokuwa imewabeba vijana watatu ilijiburura pale ambapo mmoja wao alishuka na kumyooshea Sanga mtutu wa bastola akimuamrisha kufanya chaguo la kutoa kila kitu alichokuwa nacho mfukoni ama aondoke na uhai wake.
Kwa kuogopa na ugeni wake nchini Kenya, Sanga alitetereka na kuingia mfukoni ambapo alitoa simu zote tatu alizokuwa nazo, pesa taslim elfu 27 na ufunguo wa gari na kumkabidhi mwizi huyo aliyefurahi kweli kupata ‘mteja’ mtiifu kama raia huyo wa Tanzania.
Lakini hakuwa anajua kwamba amewekwqa mtegoni ambapo aling’ang’ana kubeba bidhaa zile zote kwa mikono yake miwili na hivyo kusahau kushikilia bastola yake kwa ustadi na Sanga akachukua hiyo fursa na kumpokonya bastola ile kabla ya kuanza kumshambulia.
Kwa bahati mbaya Sanga ambaye alikuwa mgeni wa kutumia silaha ile hakuweza kumfuma vizuri baada ya kumlenga lakini aliweza kumjeruhi mwizi huyo kwa silaha yake mwenyewe ambapo aliacha kila kitu na kukimbilia maisha yake pindi alipoona kwamba silaha yake imemgeuka na sasa ilikuwa ikifukuzia roho yake.
Polisi waliofika katika eneo hilo la tukio walipata matone ya damu ishara kwamba japo Sanga hakumlenga vizuri mwizi huyo lakini alimjeruhi vya kutosha.
Uchunguzi ulianzishwa na msako mkali ili kumtafuta mwizi huyo aliyekwepa kifo cha silaha yake. DCI walimsifia raia huyo wa Tanzania kwa kitendo chake cha ujasiri.