Rais wa zamani wa Honduras amepelekwa Marekani ili kukabiliwa na madai ya ulanguzi wa madawa ya kulevya, chini ya miezi mitatu tu baada ya muhula wake kukamilika.
Juan Orlando Hernandez amekabidhiwa kwa maafisa wa Marekani wa kitengo cha kukabiliana na mihadarati katika uwanja wa ndege ulioko katika mji mkuu Tegucigalpa.
Hernandez mwenye umri wa miaka 53 mbali na madai ya ulanguzi wa mihadarati atakabaliwa na mashtaka ya kusafirisha silaha Marekani kinyume cha sheria.
Anadaiwa kusaidia katika ulanguzi wa kilo laki tano za madawa ya kulevya ya cocaine kutoka Honduras hadi Marekani.
Hernandez anakanusha mashtaka hayo. Anasema walanguzi wa madawa ya kulevya wanaotaka kupokea kifungo cha muda mfupi Marekani ndio waliompangia njama hiyo.