Rais Samia ashinda tuzo Afrika
RAIS Samia Suluhu Hassan ameshinda Tuzo ya Mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye kwa mafanikio ya serikali yake katika ujenzi wa miundombinu ya usafi rishaji.
Tuzo hiyo hutolewa kwa watu mashuhuri barani Afrika ambao wameonesha dhamira ya kuendeleza miundombinu ya usafiri katika bara hilo. Hayo yalibainishwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika taarifa yao kwa vyombo vya habari jana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia alitangazwa jana mjini Abidjan nchini Ivory Coast kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka huu. “Kamati ya uteuzi ilimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake binafsi, uwekezaji mkubwa na kujitolea katika kupanua mtandao wa barabara na reli nchini Tanzania.
Tunatuma pongezi zetu za dhati kwa Rais Samia na wananchi wa Tanzania,” ilisema taarifa hiyo. AfDB ilisema Kamati ya Uteuzi ilibaini kuwa kiasi cha Dola milioni 290 zilitolewa na benki hiyo kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa barabara, reli na usafiri wa anga Tanzania pamoja na kuzingatia mkataba wa Dola za Marekani milioni 172.2 uliosainiwa na Kampuni ya China (China Corporation Limited) kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa ya mizigo 1,430 ili kutekeleza mpango kabambe wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Aidha, kamati pia ilibaini kuanza kwa ujenzi wa Mradi wa Barabara ya Mzunguko katika Jiji la Dodoma, ambao ulizinduliwa na Rais Samia Februari mwaka huu na kushuhudiwa na Rais wa AfDB, Dk Akinwumi Adesina. Rais Samia aliingia madarakani Machi mwaka jana kutokana na kifo cha Rais John Magufuli.
Baada ya kuingia madarakani, Rais Samia aliweka bayana kuwa atakamilisha ujenzi wa miradi yote ikiwemo ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano, lakini pia serikali yake itaanzisha miradi mipya.
Baadhi ya miradi hiyo ni ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja la Tanzanite Dar es Salaam, ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani, ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi mkoani Mwanza, ujenzi wa Daraja la Wami, ujenzi wa Barabara ya Kidatu-Ifakara, ujenzi wa barabara ya mwendokasi kutoka Mbagala hadi Gerezani Kariakoo.
Miradi mingine ni ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato jijini Dodoma, viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali, ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Morogoro-Dodoma- Makutupora, Mwanza- Isaka na vipande vingine vilivyobaki pamoja na miradi mbalimbali ya barabara.
Ikifadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Tuzo ya Africa Road Builders Babacar Ndiaye’ inaandaliwa na Acturoutes, Jukwaa la Habari kuhusu miundombinu na barabara katika Afrika na Taasisi ya Vyombo vya Habari kuhusu Miundombinu na Fedha Afrika (MIFA), ambao ni mtandao wa waandishi wa habari Afrika waliojikita katika miundombinu ya barabara.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari alishinda tuzo hiyo mwaka jana. Tuzo hiyo ilianzishwa kwa heshima ya Babacar Ndiaye, Rais wa Kundi la Benki ya Maendeleo Afrika kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.
Tuzo kwa mwaka 2022 inayokwenda kwa Rais Samia itakabidhiwa katika mkutano wa mwisho wa Africa Road Builders uliopangwa kufanyika sambamba na mkutano wa mwaka wa AfDB mwezi ujao mjini Accra, Ghana.