RAIS Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Afya kuchunguza haraka mifumo inayotumiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hasa ufuatiliaji wa dawa tangu zinapotoka hadi pale zinapofika kwenye vituo.
Rais Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi wa M-MAMA, Dolorosa Duncan (kulia), kuhusu mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga M-MAMA, kabla ya kuuzindua, jijini Dodoma jana. PICHA: IKULU
Samia alitoa agizo hilo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa kitaifa wa mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga (m-mama).
Agizo hilo amelitoa ikiwa takriban ni wiki moja tangu alipoweka bayana kwamba taasisi hiyo inapaswa kusukwa upya ikiwa ni pamoja na kufumua uongozi mzima na kuweka watu wapya. Alisema hayo baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo pamoja na mambo mengine, ilionyesha upungufu katika utendaji kwenye taasisi hiyo.
“Naomba niwaahidi Watanzania kutoa au kujenga kasi ya mfumo wa huduma bora za afya. Tumeanza kulifanyia kazi hilo kutoa huduma bora za afya kama alivyosema Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu). Tumeanza na ujenzi wa miundombinu ambapo vituo kadhaa ngazi ya vijiji, kata, wilaya na ngazi za mikoa na kazi ya kununua na kusambaza vifaa tiba inaendelea.
“Upatikanaji wa dawa tumetoa mabilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini kuna mapungufu (upungufu) na juzi nilipotoa agizo kwa wizara kuangalia masuala ya mifumo nilitoa pia agizo la kuiangalia MSD kwa haraka sana. Najua sehemu moja ni yangu na nakuahidi kwamba nitaifanya kwa haraka lakini kwenye mifumo ya kutoa huduma ni sehemu yako, naomba mkaifanyie kazi haraka sana na zaidi ule mtandao wa kuifuatilia dawa mpaka pale inapofika.
Ukiharakishwa itakuwa vizuri zaidi,” alisema.
Pia alisema serikali imejitahidi kuajiri watumishi katika sekta ya afya na kwa mwaka jana, watumishi 3,600 waliajiriwa.
“Na kwa mwaka huu uchumi wetu umeturuhusu kuajiri watumishi 32,000 ndani ya taifa letu ambao kati ya hizo nyingi zitakwenda katika sekta ya afya na elimu bila shaka” alisema.
Kadhalika alisema pamoja na kuanzishwa kwa mfumo huo wa m-mama serikali imehakikisha maeneo yote yanakuwa na magari ya kubeba wagonjwa angalau kila kata gari moja.
“Tumeagiza ‘ambulance’ (magari ya kubeba wagonjwa) 233 za kawaida ambazo zitamwagwa Tanzania nzima lakini pia tumeagiza ‘ambulance’ 25 ambazo ni ‘advance’ hizi ni kama ngazi ya rufani. Kama zile zinakuwa hazitoshi au hazina vifaa basi hizi 25 zitatumika lakini pia tumeagiza magari 242 ya uratibu ni matumaini yangu kwamba magari na ‘ambulance’ hizi zitakwenda kuongeza nguvu kwenye huu mpango wa m-mama ili kuwawahisha watoto na kinamama hospitalini,” alisema.
Rais pia alisema kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) serikali katika mwaka wa fedha uliopita imetoa fedha nyingi ili kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini na kurahisisha utoaji wa huduma za afya.
Rais Samia aliipongeza kampuni ya simu za mkoani ya Vodacom kwa kuwezesha mfumo huo wa m-mama ambao utasaidia kuratibu usafiri kwa ajili ya wajawazito na watoto wachanga kupitia magari ya kubeba wagonjwa yaliyosajiliwa na magari binafsi.
Waziri Ummy alimpongeza Rais Samia kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika kuboresha sekta ya afya kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha.
Ummy alisema hivi sasa wanapanga kufanya mazungumzo na Vodacom ili kutengeneza mfumo utakaosaidia kufuatilia usambazaji wa dawa kutoka MSD hadi katika vituo vya afya.
Alisema lengo la serikali ni kutekeleza mpango wa m-mama nchi nzima ili kukomesha vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo, alisema bunge litaendelea kuipa serikali ushirikiano katika kuwaletea wanachi maendeleo.