Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania haitajengwa na mtu mmoja au chama kimoja bali itajengwa na Watanzania wote.
Rais Samia ameeleza hayo leo Jumanne Aprili 5, 2022 Jijini Dodoma wakati akizindua mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), unaojadili maridhiano, haki na amani.
“Tulichagua kuingia mfumo huu wa vyama vingi tukijua kwamba ndani ya mfumo huu tutakwenda kupata maendelo ya haraka kwa sababu vyama viko vingi, macho yako mengi, maono yapo mengi wanavyoona chama kimoja ambacho kipo ndani ya serikali pengine hawatokuwa na macho makubwa ya kuona kama wengine walio nje ya Serikali, na ndio maana tukasema vyama vingi hivi kazi yake ni kuangalia yanayoendelea ndani ya Serikali na kutoa maoni yao, jamani hivi tunakwenda hivi, lakini mbona mmh, mbona tunaona hivi, mbona sheria hii ingebadilishwa hivi, mbona sera hii tungekaa tukazungumza hivi.
“Tanzania haitajengwa na mtu mmoja na chama kimoja. Wote kama Watanzania lazima tujadili mambo yetu iwe sera, sheria, dira lazima tujadili wote kama Watanzania.
"Tukikubaliana, tunakwenda kutekeleza wote kama Watanzania. Atakayekiuka hapo ni mkosaji, awe ametoka kokote kule kwa sababu tulijadiliana na kukubaliana tunaiweka hivi na hiyo ndio itakayokwenda kutuongoza katika utendaji wetu na maisha yetu kwanza ushirikishwaji kutoka serikalini ni uhakika “ Rais Samia Suluhu Hassan