Mei 28, 2018, mwanasiasa mwandamizi nchini, Abdulrahman Kinana aliandika barua ya kujiuzulu ukatibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Aprili Mosi, 2022 Kinana amerejea kwenye chama akiwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.
Piga hesabu. Kutoka Mei 28, 2018 mpaka Aprili Mosi, 2022 ni miaka mitatu, miezi 10 na siku nne. Yaani siku 1,404. Huo ndio muda ambao Kinana alikuwa nje ya CCM.
Ni kwa nini amerejea CCM? Hilo swali lazima liambatane na linalohoji kwa nini aliamua kujiuzulu? Bila shaka muktadha wa kimazingira na uchambuzi wa nadharia, vinaweza kutusogeza kwenye jibu.
Tengeneza awamu, kipindi gani Kinana aliingia CCM kuwa Katibu Mkuu? Jibu ni wakati Mwenyekiti wa chama hicho akiwa Jakaya Kikwete. Aliondoka nyakati ambazo chama kinaongozwa na Dk John Magufuli. Amerejea usukani wa CCM ukishikiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Unaweza kujiuliza Kikwete na Rais Samia wana kipi cha kuwafanya wafanane hadi kumvutia Kinana? Jiulize pia upekee wa Magufuli dhidi ya wenzake hao hadi Kinana akaona hawezi kuendelea kufanya naye kazi.
Kinana aliyefanya kazi na Kikwete alikuwa ndiye injini ya chama. Zipo taarifa kwamba alitumia mpaka rasilimali zake binafsi kuzunguka mikoa, wilaya, majimbo, kata na vijiji ili kukijenga chama. Alikatiza porini na kuvuka mito, maziwa na bahari kukipa uhai chama.
Kinana alikuwa mwenye kukisemea chama hasa. Alikuwa tayari kugombana na mawaziri wa Serikali iliyoongozwa na mwenyekiti wake (Kikwete) ili kuwafanya wananchi waone kwamba CCM ni chama chenye kujali na kutetea masilahi ya umma. Alitaka ionekane kuwa makosa ya Serikali chanzo chake siyo CCM.
Kinana chini ya Kikwete alitaka mawaziri wawajibike kwenye chama. Kibao hicho cha Kinana kimerejea. Hotuba yake mara tu alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, ameweka wazi azma yake ya kutaka Serikali iwe inahojiwa na kujieleza mbele ya chama kwa kuwa ndicho huomba kura kwa wananchi.
Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, na hasa Magufuli aliposhika usukani wa chama Kinana alibadilika. Hakuwa yule vuguvugu za majukwaani, wala hakuonekana popote akikisemea chama.
Kinana akibaki kuwa Katibu Mkuu chini ya Magufuli, alikuwa jina tu. Masuala yote ya chama aliyaacha kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.
Mei 30, 2018 mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, Magufuli alisema kuwa Kinana aliomba kujiuzulu mara nyingi tangu mwaka 2016 mpaka Mei 28, 2018, alipoamua kumkubalia.
Hapo jawabu unalo kuwa Kinana hakuwa na utayari wa kuendelea kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kipindi kikiwa chini ya Magufuli, ndio maana aliomba kwa msisitizo wa mara kwa mara kujiuzulu. Rejea kauli ya Magufuli.
Hoja ni tabia?
Katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM mwaka 2016, Kikwete alipokuwa anakabidhi rungu la chama, Kinana alimpamba mno Rais huyo wa nne wa Tanzania. Alisema, Kikwete ni mtu mwenye roho nzuri, mpole na mkarimu.
Yupo mtu anaweza kusema kuwa Kikwete na Kinana walielewana kwa sababu historia ya muda mrefu pamoja na wote ni wanajeshi. Hata hivyo, Samia si mwanajeshi lakini mbona amerudi?
Je, hoja haiwezi kuwa jinsi chama kilivyoendeshwa? Ndiyo, wakati wa Kikwete CCM ilionekana ipo kwenye misingi yake. Waliposemwa wenyewe walionekana na wakibadilishana awamu kwa awamu.
Uteuzi wa viongozi
Wakati wa Magufuli, chama kilionekana kuchepuka katika njia zake. Uteuzi wa Polepole kuwa Katibu Mwenezi ulikifanya chama kionekane kinaacha hatamu zake kushikwa na wageni ambao historia zao ndani ya taasisi hazina mizizi yoyote.
Katika hili la viongozi wa CCM kutokuwa na mizizi kwenye chama, lilimgusa mpaka aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ally. Wapo watu wamewahi kumtuhumu waziwazi kwamba ana kadi ya uanachama wa Chama cha Wananchi (Cuf).
Wabunge wa upinzani
Lipo suala la wabunge wa upinzani kuhamia CCM kwa hoja ya kuunga juhudi za Rais Magufuli, kisha wakapitishwa bila kupingwa kutetea majimbo yao. Hata hili lilisababisha mafuriko ya wageni.
Mgeni alijiunga na chama, wenyeji wakazuiwa kushindana naye ili akatetee kiti chake. Matokeo yake wahamiaji wakawa wanatamba, wenye historia na chama wakabaki kuumia chini kwa chini kwa kuwa waliogopa kuraruliwa na Simba aliyekuwapo madarakani.
Wazee wa chama wakawa hawatambuliki tena. Hata heshima ya ustaafu hawakupewa. Vijana wasio na nafasi yoyote ya uongozi kama Cyprian Musiba, wakawa ndio wasemaji na wanaotuhumu watu mbalimbali.
Zipo nadharia kuwa moja ya mambo yaliyomuumiza zaidi Kinana na kushinikiza kuachia ukatibu mkuu ni ujio wa wabunge na kuibuka kwa akina Musiba kama wasemaji wa chama.
Ikumbukwe kuwa Julai 2019, kipindi Kinana akiwa ameshaondoka CCM, akishirikiana na Katibu Mkuu wa chama hicho wa mwaka 2006 mpaka 2011, Yusuf Makamba waliandika waraka wakilalamika kuchafuliwa na Musiba pasipo chama kuingilia kati.
Kinana wa Samia
Kinana ni mwanasiasa msomi na mwenye uzoefu mkubwa wa kiuongozi. Ni mwanajeshi aliyepanda ngazi hadi cheo cha kanali. Ameshakuwa mbunge na mjumbe wa Baraza la Mawaziri kwa vipindi tofauti. Vilevile ni Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki.
Ameshaitumikia sana nchi. Na kwenye chama, alikuwepo Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League), akawa mwalimu wa siasa jeshini. Aliongoza kampeni za urais za Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa na Kikwete. Alikuwa Katibu Mkuu aliyewaingiza Magufuli na Samia madarakani.
Utendaji kazi wa Kinana ni kivutio kwa viongozi wengi wakubwa CCM, akiwemo Mkapa. Mwandishi wa makala haya alifanikiwa kuiona barua ambayo Mkapa alimwandikia Kinana mara baada ya kuachia ukatibu mkuu.
Mkapa alimwambia Kinana kuwa alihuzunika kuona anastaafu ukatibu mkuu kwa kuwa alishuhudia akifanya kazi kubwa kukiimarisha chama kilichokuwa kimeanza kupoteza umaarufu, na namna alivyoratibu mchakato wa kupata mgombea urais mwaka 2015.
Mkapa alifanya kazi na Kinana, kama Kikwete. Wote walivutiwa naye. Ilifika hatua Kikwete alipendekeza jengo la mikutano CCM, Dodoma la Jakaya Kikwete, lipewe jina la Kinana. Hata hivyo, ikaamuliwa liitwe Jakaya Kikwete.
Je, Rais Samia ameona kwa vile Kinana ni komredi aliyekubalika kwa watangulizi wake wengine ndio maana ameona naye afanye naye kazi? Ni kwa nini Kinana naye amekubali?
Safu ya uongozi CCM
Tangu Samia aliposhika usukani wa uongozi wa chama, ni wazi amechagua kukirejesha chama kama msingi waliopita nao akina Kikwete na Mkapa.
Kwanza ni muundo wa sekretarieti ya chama. Kuanzia Katibu Mkuu, Daniel Chongolo ambaye ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti na wajumbe wake wote wa sasa, kila mmoja angalau ana historia na chama.
Kwa jinsi Rais Samia alivyounda safu yake ya uongozi kwenye chama, jumlisha na maneno yake, bila shaka kuna masahihisho anakusudia chama kiyafanye ambayo anaona yalifanywa nyakati zilizopita.
Je, Samia ameona Kinana ndiye mtu mwafaka wa kufanya masahihisho hayo kwenye chama? Je, Kinana ameridhia kurejea kwenye chama kwa sababu ameona Samia anaendana naye na ameyaelewa masahihisho anayotaka yafanyike?
Katiba ya CCM inaitambulisha nafasi ya Makamu Mwenyekiti kuwa ya ushauri zaidi. Hata hivyo, kwa hali iliyopo, kama kweli kuna masahihisho yanatakiwa kufanyika na Kinana ameonekana ndio mleta mageuzi, ni wazi kuna kazi kazi kubwa anatakiwa kufanya.
Swali ni je, Kinana wa Samia kama Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, anafanya kazi kwa msuli mkubwa kama yule Katibu Mkuu chini ya Kikwete?
Mwananchi