Rungu Jipya la Meya Raibu Aliyevuliwa Umeya Moshi Linakuja




Moshi. Mambo yanazidi kumwendea kombo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu aliyevuliwa wadhifa huo juzi, baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuthibitisha inamchunguza.

Wakati Takukuru ikithibitisha kumchunguza kiongozi huyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimedai kusikitishwa na kauli ya Raibu kuwahusisha viongozi wake na kuondolewa kwake wakati suala hilo ni la kiserikali.

Raibu alipigiwa kura juzi katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, Manispaa ya Moshi ambapo kura 18 ziliafiki ang’olewe katika nafasi hiyo kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali, huku kura 10 zikimkingia kifua aendelee kuwa Meya.

Baadhi ya tuhuma zilizomng’oa ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi, kuruhusu ujenzi holela eneo la kibiashara katikati ya mji (CBD) katika mazingira ya rushwa na mienendo mibaya na ukosefu wa adabu kwa madiwani wenzake.


“Siwezi kuwaingilia katika hili, lakini baadhi ya viongozi wa chama Mkoa na Wilaya wameingilia suala hili kuhakikisha naondolewa kwa sababu nimeingilia maslahi ya chakula chao,” alisema Raibu baada ya kung’olewa.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Takukuru mkoa Kilimanjaro, Frida Wikes alisema Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro walipokea taarifa na tuhuma kadhaa zinazomkabili Raibu na kwamba wanaendelea kuzifanyia kazi na kukataa kuingia kwa undani aina ya tuhuma zinazochunguzwa na taasisi hiyo.

Akizungumza jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema utaratibu wa kumuondoa Meya madarakani ulifanywa na Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro na Halmashauri na chama hicho hakihusiki.


“Tumesikia maamuzi yaliyochukuliwa na baraza na tumesikia tuhuma dhidi ya viongozi wa CCM. Tutakutana kutafakari kwa mujibu wa kanuni na katiba ya chama, tukiona kuna sababu ya kushughulikia tutalishughulikia na tutatoa taarifa,” alisema Mabihya.

Amri ya Meya kuhusu barakoa

Januari 28, 2021 dunia ikiwa katikati ya mapambano ya ugonjwa wa Uviko-19, Meya Raibu aliwasimamisha wananchi wanne waliokuwa ndani ya ukumbi wa Manispaa wakifuatilia kikao cha baraza na kuwaamuru kuvua barakoa, kitendo kilichowakera wataalamu wa afya na wananchi. Raibu pia aliwahi kutajwa kwenye sakata la mfanyabiashara Elioth Lyimo, aliyedai kuchukuliwa fedha zake Sh25 milioni na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kwamba wakati akizichukua, alikuwa na Raibu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad