Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Samia Suluhu Hassan ametaja sababu iliyomfanya Mzee Philp Mangula kuandika barua ya kuomba kung'atuka katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara.
Rais Samia na Mwenyekiti wa CCM wakati akiisoma barua ya Mzee Mangula kwenye Mkutano Mkuu wa CCM leo April Mosi, 2022 makao Makuu ya chama hicho Jijini Dodoma, amesema kuwa moja ya sababu zilizomfanya Mzee Mangula kung'atuka ni Umri ambapo ameeleza kwenye barua hiyo kwamba umri mkubwa alionao unamfanya wakati mwingine ashindwe kutekeleza majukumu yake katika chama kama inavyotakiwa.
Wakati akiisoma barua hiyo mbele ya wajumbe wa Mkutano huo, Rais Samia amesisitiza kwamba Mzee Mangula ameng'atuka na siyo kujiuzuru nafasi yake. Aidha katika barua hiyo mzee Mangula ameeleza pia sehemu alizowahi kukitumikia chama chake na serikali kazi ambayo ameifanya kwa kipindi chote cha utumishi wake.
Hata hivyo, ili kuziba nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi nafasi iliyoachwa wazi na Mzee Mangula. Mwenyekiti wa CCM amewaeleza wajumbe wa mkutano Mkuu ulioketi leo kuwa, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa umempendekeza Kanali Abdulrahman Omari Kinana kugombea nafasi hiyo na akawaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya zoezi hilo. Uchaguzi huo unafanyika leo katika Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.